Mapambano bado yaendelea Sudan Kusini
29 Januari 2014Umoja wa Mataifa umesema idadi ya raia wanaotafuta hifadhi katika kambi zake nchini humo inazidi kupanda. Naibu wa msemaji wa umoja wa Mataifa Fahran Haq amewaambia waandishi wa habari kuwa kikosi cha kulinda amani cha umoja wa Mataifa kilichoko Sudan Kusini, UNMISS, kimeripoti kuzorota kwa hali ya usalama katika baadhi ya maeneo ya jimbo la Unity ambako kuna viwanda muhimu vya mafuta na mapigano ya mara kwa mara yameripotiwa kati ya wanajeshi na waasi wanaomuunga mkono aliyekuwa makamu wa Rais Riek Machar. Haq amesema idadi ya watu waliopewa hifadhi katika kambi za Umoja wa Mataifa kote nchini humo imeongezeka na kufikia watu 79,000 kutoka idadi ya awali ya 76,000. Nusu ya idadi hiyo iko kazika kambi mbili za Umoja wa Mataifa mjini Juba.
Raia wengi wa Sudan Kusini wanaendelea kutoroka nchini humo kutokana na hofu kwamba makubaliano ya kusitisha vita huenda yasitekelezwe. Huyu hapa ni mmoja wa raia wanaoishi katika kambi ya wakimbizi nchini Uganda. "Bado kuna dalili za kuendelea mapigano, licha ya muafaka wa kusitisha mapigano. Serikali haitaki kuwapa waasi nafasi yoyote, nao waasi wanataka madaraka, na watajaribu wawezavyo kujipanga upya na kushambulia. Kwa hivyo kuna hofu mapigano yanaweza kuanza tena"
Takribani watu 47,000 wamepewa hifadhi nchini Uganda na msemaji wa Shirika la Kuwashughulikia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa nchini Uganda Lucy Beck anasema hali ni mbaya katika kambi hizo."Kufikia jana walikuwa karibu 197, lakini wale wanaowasili ni wanyonge baada ya kusafiri kwa muda mrefu bila pesa za kutosha. duru nchini Sudan Kusini zinasema kuna watu wengi ambao hawajafanikiwa kufika Uganda, au wangali njiani".
Mkuu wa shirika la misaada ya kibinadaaamu wa Umoja wa Mataifa Valerie Amos ambaye hapo jana alizuru mji wa Malakal amesema uhalifu wa kivita umefanyika Sudan Kusini na kuongeza kuwa watu aliozungumza nao wamepoteza kabisa imani na wanataka kuhamishwa hadi maeneo mengine nchini humo au hata katika nchi nyingine. Mashirika ya kutoa misaada nchini humo yamesema kiasi ya watu 10,000 wameuawa katika mzozo huo ulioanza tarehe 15 mwezi uliopita.
Na wakati hali ikiendelea kuwa tete nchini humo, Waziri wa sheria wa Sudan Kusini Paulino Wanawilla Unago amesema kuwa kiongozi wa waasi Riek Machar na wenzake sita wanastahili kushtakiwa kwa makosa ya uhaini kuhusiana na jukumu lao katika umwagaji damu uliofanywa nchini humo. Waziri huyo amesema wanasiasa wengine saba waliokamatwa baada ya vurugu kuzuka, wataachiliwa huru, ikiwa ni mojawapo ya masharti ya waasi katika meza ya mazungumzo.
Miongoni mwa wale waliowekwa kizuizini ni Pagan Amum, ambaye alikuwa katibu mkuu wa chama tawala, aliyekuwa waziri wa usalama wa taifa Oyai Deng Ajak, balozi wa zamani nchini Marekani Ezekiel Lol Gatkuoth na aliyekuwa naibu waziri wa ulinzi Majak D'Agoot.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman