Mapambano ya kisiasa hayajapoa Venezuela
13 Februari 2019Kiongozi huyo wa upinzani nchini Venezuela akiwa amezungukwa na umati mkubwa wa wafuasi wake waliokuwa wakimshangilia alitangaza kwamba tarehe 23 mwezi huu itakuwa siku ya kuupeleka msaada unaotakiwa haraka nchini Venezuela kutoka Marekani ambao umekwama mpaka sasa katika mpaka wa Colombia tangu wiki iliyopita ukisubiri kuingizwa nchini Venezuela ambako utawala wa rais Maduro unazuia harakati za kiongozi huyo wa upinzani.
Hata hivyo Guaido hakutowa maelezo kuhusu jinsi msaada huo utakavyoingizwa Venezuela kutokea mji wa Cucuta nchini Colombia ingawa amesema ataongoza msafara wa magari kupeleka msaada huo,hali ambayo inatajwa kwamba inawezekana kusabisha hatari inayoweza kuleta vurugu zaidi na mapambano na vikosi vya usalama
Kiasi watu 40 wameshauwawa katika mapigano nchini humo tangu kiongozi huyo wa upinzani mwenye umri wa miaka 35 kujitangaza rais wa mpito Januari 23.Guaido amezungumza katika mahojiano maalum aliyofanyiwa na Dw na kusema muda unayoyoma kwa utawala wa rais Nicolas Maduro.
''Utawala wa Maduro unaishiwa na muda.Utawala huu hauna mustakabali kwasababu Maduro hana mapendekezo na haungwi mkono na wananchi,hana mwelekeo. Hawalindi wananchi wake na hilo ni jambo ambalo linakwenda kinyume na vuguvugu linaloungwa mkono na watu wengi na kuungwa mkono na jumuiya ya Kimataifa. Pia ni vuguvugu lenye mipango kwa taifa,lina mipango ya kuleta ustawi Venezuela. Haliwezi kuzuilika. Inachoweza kufanya serikali ya Maduro ni kimoja tu ambacho wanakijua zaidi nacho ni kukandamiza,kutesa,kufunga watu au kuzinyakua fedha za Venezuela. Lakini ambacho hakiwezi kuzuilika ni kwamba tutakuwa na kipindi cha amani cha mpito kinachozingatia demokrasia nchini Venezuela kwa ajili ya ubora wa wananchi wetu.''
Katika uwanja wa Kimataifa Guaido anaungwa mkono na takriban nchi 60 ikiwemo Marekani ambayo imeshaahidi kutoa dolla milioni 20 kuisaidia Venezuela na pia imeshatuma dawa na chakula hicho kilichokwama kwenye eneo la mpaka kati ya Venezuela na Colombia.
Washauri wa kiongozi huyo wa upinzani wanamtaka pia ateue watendaji wakuu sita kulisimamia shirika pekee muhimu la shughuli za usafishaji mafuta Citgo lililoko nje ya Venezuela. Shirika hilo linatajwa kwamba limeingia kwenye migawanyiko kufuatia mapambano ya kisiasa.
Mwandishi:Saumu Mwasimba
Mhariri: Iddi Ssessanga