Mapigano yaendelea Sudan licha ya mkataba wa kuyasitisha
29 Aprili 2023Licha ya kuwepo makubaliano ya kurefusha usitishaji mapigano, mashambulizi ya anga na mizinga ya vifaru vimeendelea kusikika usiku kucha wa kuamkia siku ya Jumamosi kwenye mji mkuu wa Sudan, Khartoum, na mji wa jirani uitwao Bahri.
Makabiliano hayo yameuweka rehani mkataba wa kuacha kupigana kwa saa 72 zaidi uliofikiwa kati ya vikosi vya jeshi la taifa na wapiganaji wa kikosi cha wanamgambo wenye nguvu cha RSF.
Wingu la moshi mzito lilitanda kwenye viunga vya mji wa Khartoum huku milio ya risasi na makombora vikisikika kwenye maeneo ya makaazi. Jeshi limekuwa liitumia ndege za kivita ikiwemo zisizo na rubani kuzishambulia ngome za RSF mjini Khartoum.
Ikumbukwe mapigano hayo yanahusisha vikosi vinavyomtii mkuu wa jeshi na kiongozi wa taifa, Abdel Fattah al-Burhan, dhidi ya vile vya hasimu wake Mohamed Hamdan Daglo anayeongoza kikosi RSF.
Hofu imetanda kwa wakaazi wa mji mkuu, Khartoum
Wengi ya wakaazi wa mji wa Khartoum na viunga vyake wamezingirwa na mapigano makali wakiwa hawana chakula, maji, mafuta na hata umeme .
Mkaazi mmoja aliyejitambulisha kwa majina ya Mahasin al-awad amesema wamekuwa wakisikia mingurumo ya ndege za kivita na makombora na wengi ya waakazi mjini Khartoum ikiwemo yeye binafsi, wana wasiwasi mkubwa juu ya maisha yao.
Hadi sasa watu wasipungua 512 wamepoteza maisha na wengine zaidi ya 4,200 wamejeruhiwa tangu kuzuka kwa machafuko hayo nchini Sudan mnamo April 15 .
Takwimu hizo ni kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa. Kwa upande wake asasi ya madaktari wasio na mipaka imesema mapiganao hayo yamesababisha vifo vya raia 387.
Umoja wa Mataifa umearifu kwamba mapigano mengine yanaendelea kwenye mitaa ya jimbo la Darfur ambalo tangu mwanzo tayari limeharibiwa kwa vita.
Inaaminika watu wasipungua 96 wamepoteza maisha huko Darfur kutokana na mapambano hayo. Pande zinazopigana kila mmoja amemlamu mwengine kuwa chanzo cha kukiuka masharti ya kusitisha mapigano.
Kila upande unamlaumu mwingine kuwa chanzo cha mapigano
Kikosi cha RSF kimesema jeshi ndiyo limeshindwa kuheshimu mkataba wa kusitisha mapigano kwa kufanya mashambulizi ya anga kwenye kambi zake katika mji wa Omdurman unaopakana na Khartoum.
Jeshi nalo limesema ni vikosi vya RSF ndiyo vimetibua usitishaji mapigano. Mkataba huo wa kusitisha vita ulipaswa kuheshimiwa hadi usiku wa manane wa Jumapili.
Katika hatua nyingine Umoja wa Mataifa umetoa tahadhari kuhusu wafungwa, ambao ni washukiwa wa uhalifu, kutoroka magereza nchini Sudan huku kukiwa na ghasia zinazoendelea nchini humo.
Msemaji wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya haki za Binadamu, Ravina Shamdasani, amewambia waandishi wa habari mjini Geneva kuwa wamesikitishwa sana na taarifa za wafungwa kutoroka magereza.
Matamshi yake yanafuatia wafungwa kutoroka jela kadhaa, tangu ghasia kuzuka kote Sudan wiki mbili zilizopita, ikiwa ni pamoja na gereza lenye ulinzi mkali linalowashikilia washukiwa wahalifu wa kivita.