Mapigano yanaendelea katika mji wa Khartoum nchini Sudan
7 Mei 2023Mapigano yanaendelea katika mji wa Khartoum licha ya juhudi za hivi karibuni zinazoungwa mkono na Saudi Arabia na Marekani za kusimamisha mapigano hayo. Mashambulio ya bunduki na ndege yalifumuka tena leo katika mji huo. Vita hivyo kati ya pande mbili za jeshi la Sudan vilianza kati kati ya mwezi uliopita na tayari watu wapatao 700 wameshauawa, wengi wao wakiwa raia. Maalfu wengine wameikimbia nchi. Mazungumzo juu ya kuyasimamisha mapigano hayo yanaendelea mjini Jeddah, Saudi Arabia kati ya wajumbe wa pande mbili za jeshi la Sudan pamoja na wapatanishi wa kimataifa. Majenerali wanaoongoza pande zinazopigana wamelaumiana juu ya kufumuka kwa vita hivyo. Msemaji wa upande wa jeshi kuu ameeleza kuwa mazungumzo ya mjini Jeddah yanahusu njia itakayowezesha kutekelezwa hatua ya kusimamisha mapigano kwa usahihi kwa manufaa ya raia. Naye jenerali wa kikosi hasimu, cha RSF Mohammed Hamdan Dagalo amesema anakaribisha kufanyika mazungumzo hayo kwa jumla.