Marekani: Hatuna mpango wa kupeleka wanajeshi nchini Ukraine
28 Februari 2024Msemaji wa baraza la usalama la kitaifa la Marekani Adrienne Watson amesema katika taarifa kuwa Rais Joe Biden ameshaweka wazi kuwa Washington haitotuma wanajeshi kupigana nchini Ukraine.
Kauli sawa na hiyo imetolewa pia na Ujerumani, Uingereza, Poland na Jamhuri ya Czech zilizojiweka mbali na pendekezo lolote la kutuma wanajeshi nchini Ukraine.
Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesema hakujakuwa na mabadiliko yoyote katika msimamo uliokubaliwa kuwa hakuna nchi yoyote ya Ulaya au nchi mwanachama wa NATO itakayopeleka wanajeshi wake nchini Ukraine.
Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Boris Pistorius amesisitiza kauli ya Scholz.
"Kupeleka wanajeshi nchini Ukraine sio chaguo kwa Ujerumani," Pistorius amewaambia waandishi wa habari wakati wa ziara yake mjini Vienna.
Soma pia: NATO: Kusaidia Ukraine ni uwekezaji wa usalama wetu
Katibu Mkuu wa muungano wa kujihami wa NATO Jens Stoltenberg amekanusha kwamba wanazingatia kutuma wanajeshi kwenye uwanja wa mapambano nchini Ukraine. Stoltenberg hata hivyo, ameeleza kuwa muungano huo wa NATO utaendelea kuiunga mkono Ukraine licha ya nchi hiyo kutokuwa mwanachama wa NATO.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron siku ya Jumatatu alieleza kuwa, hataondoa uwezekano wa mataifa ya Magharibi kupeleka wanajeshi nchini Ukraine siku za usoni japo alisisitiza kutokuwepo na mwafaka kuhusu suala hilo.
Ikulu ya Kremlin imeonya kuwa hatua yoyote ya kujaribu kupeleka wanajeshi wa mataifa ya Magharibi nchini Ukraine itasababisha mzozo kati ya Urusi na muungano wa kujihami wa NATO.