Marekani yalaani mauaji ya wanachama 2 wa upinzani Msumbiji
22 Oktoba 2024Serikali mjini Washington imejiunga na Umoja wa Ulaya na mkoloni wa zamani wa Msumbiji Ureno katika kulaani mauaji hayo na kutoa wito wa kufanyika haraka uchunguzi wa kina kuhusu mauaji ya wakili wa upinzani Elvino Dias na afisa wa chama cha upinzani Paulo Guambe waliouawa kwa kufyatuliwa risasi siku ya Jumamosi.
Marekani ndio mfadhili mkubwa zaidi wa Msumbiji, kwa kutoa msaada wa zaidi ya dola milioni 560 kila mwaka. Hapo jana, polisi nchini Msumbiji walifyatua mabomu ya kutoa machozi kuutawanya umati mdogo wa watu mjini Maputo huku maduka yakifungwa kutokana na maandamano ya kupinga udanganyifu katika uchaguzi.
Kiongozi wa upinzani Venancio Mondlane, aliyewania urais katika uchaguzi wa Oktoba 9, aliitisha maandamano kupinga matokeo ya mapema. Matokeo hayo yalionyesha chama tawala cha Frelimo kikiongoza.