Marekeni, Ujerumani zalaani hukumu dhidi ya Meya wa Istanbul
15 Desemba 2022Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imeelezea wasiwasi na kuvunjwa moyo na hukumu hiyo, amesema naibu msemaji wa wizara hiyo Vedant Patel, huku akihimiza utatuzi wa haraka na wa haki wa kesi hiyo.
Wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani ilisema kupitia ujumbe kwenye ukurasa wake wa Twitter, kwamba hukumu dhidi ya Imamoglu ni pigo kubwa kwa demokrasia.
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch katika taarifa yake ya leo limelaani hukumu hiyo na kuitaja kama shambulio la kisiasa linalonuwiwa kuwaweka kando au kuwanyamazisha wanasiasa wa upinzani.
Mahakama mjini Istanbul ilimuwekea Imamoglu marufuku ya kisiasa ya miaka miwili na kifungo cha gerezani cha miaka miwili na miezi saba kwa kuwatukana maafisa wa uchaguzi wa Uturuki katika hotuba yake ya mwaka 2019, madai ambayo Imamoglu anayapinga. Hata hivyo uamuzi wa mahakama hiyo siyo wa mwisho.
Meya huyo mashuhuri anachukuliwa kama anaeweza kuwa mpinzani wa Rais Racep Tayyip Erdogan katika uchaguzi wa rais na bunge unaotarajiwa kufanyika katika muda wa miezi sita ijayo.
Soma pia: Upinzani washinda umeya jiji la Istanbul
Erdogan ameiongoza Uturuki kwa miaka 20 sasa. Haikuwa wazi iwapo na ni lini hukumu hukumu dhidi ya Imamoglu itathbitishwa.
Iwapo Imamoglu atafungwa, mamlaka katika mji huo mkubwa zaidi nchini Uturuki ambao pia ndiyo mji mkuu wa kifedha, yatakabidhiwa kwa chama cha tawala cha Rais Erdogan, kilicho na wawakilishi wengi zaidi katika baraza la jiji.
Kabla ya ushindi wa Imamoglu mnamo 2019, Istanbul ilikuwa ngome kuu na chimbuko la madaraka kwa Erdogan na watangulizi wake wahafidhina wa Kiislamu kwa miaka 25.
Viongozi wa muungano wa vyama sita vya upinzani, kikiwemo kikuu cha upinzani chama Imamoglu cha Republican People's Party, CHP, walitarajiwa kuhudhuria mkutano wa mshikamano mjini Istabul leo Alhamisi.
Soma pia: Upinzani Uturuki wamtuhumu Erdogan kwa kuchochea vita
Muungano huo unaoongozwa na CHP bado haujakubaliana juu ya mgombea wao wa urais, lakini Imamoglu alikuwa anapigiwa chapuo kama anaweza kupambana dhidi ya Erdogan, na uchunguzi wa maoni unaonesha kuwa angemshinda.
Chanzo: Mashirika