Mashambulizi ya Urusi yawaua 12 Ukraine
28 Aprili 2023Rais Volodymyr Zelensky amelaani mashambulizi hayo ya makombora na yaliyofanywa na ndege zisizotumia rubani na kuapa kulipiza kisasi dhidi ya kile alichokitaja kama ugaidi wa Urusi.
Mapema leo kulishuhudiwa mkururo wa mashambulizi ya makombora na ya ndege zisizotumia rubani katika maeneo mbalimbali nchini Ukraine ambayo kulingana na Kyiv ni makubwa zaidi kushuhudiwa ambayo pia yalilenga jengo la makaazi ya watu. Haya yanafanyika siku moja baada ya viongozi wa Ukraine na China kuzungumza kwa simu, huku Xi Jinpingakiendelea kusisitiza msimamo wa China kwamba inataka amani amani kwa njia ya mazungumzo.
Kyiv, ambayo ni miongoni mwa maeneo yaliyolengwa katika mashambulizi ya mapema leo, haijakabiliwa na kadhia kama hiyo kwa zaidi ya siku 50. Waziri wa mambo ya ndani Igor Klymenko amesema mashambulizi katika mji wa Uman, kusini mwa Kyiv yamewaua watu 10, huku meya wa mji wa Dnipro Borys Filatov akiripoti watu wawili kuuawa.
Ukraine imesema ilifanikiwa kuyadungua makombora 21 kati ya 23 ya Urusi, pamoja na ndege zake mbili zisizotumia rubani usiku wa kuamkia jana.
Soma Zaidi: Shambulizi la Urusi laua mtu mmoja, 23 wamejeruhiwa Mykolaiv
Waziri wa mambo ya nje wa Ukraine Dmytr Kuleba ameandika kupitia ukurasa wa twitter kwamba hivi ndivyo Urusi inavyojibu miito yote ya kupatikana kwa amani.. kwa kuwashambulia raia wakiwa wamelala, na miongoni mwao ni mtoto wa miaka miwili.
Katika miezi ya karibuni, Urusi imepunguza kufanya mashambulizi makubwa nchini Ukraine, tofauti na wakati wa majira ya baridi ambapo ilikuwa ikishambulia pakubwa miundombinu ya taifa hilo jirani yake.
Rais Volodymyr Zelensky amelaani vikali mashambulizi haya ya karibuni na kuapa kujibu kile alichokiita ugaidi wa Urusi, wakati mapigano makali yakishuhudiwa zaidi katika eneo la mashariki mwa taifa hilo, ambako wanajeshi wanakabiliana ili kuudhibiti mji wa Bakhmut ambao kwa sasa unaonekana kama mahame baada ya kuharibiwa vibaya.
Haya yanajitokeza wakati, marais wa Jamhuri ya Czeck Petr Pavel na mwenzake wa Slovakia Zuzana Caputova wakiizuru Kyiv hii leo, hii ikiwa ni kulingana na mashirika ya habari ya CTK na TASR. Wakuu hao wawili wanatarajiwa kufanya mazungumzo na rais Zelensky na kufanya shughuli nyingine mbalimbali.
Rais wa Petr mapema leo aliyatembelea maeneo ya mji wa Bucha ambayo ni pamoja na kanisa la Mtakatifu Andrea, ambako kuna picha za wahanga wa kivita, pamoja na eneo jirani ambako raia wa Ukraine waliuawa na kuzikwa na wanajeshi wa Urusi.
"Asanteni na ninawapongeza sana kwa ujasiri na maamuzi mliyochukua ya kujitetea tangu mwanzo na bado mnajitetea hadi leo," alisema rais Petr.
Marais hawa ni miongoni mwa wanasiasa wanaoiunga mkono kikamilifu Ukraine, kisiasa na kijeshi tangu Urusi ilipoivamia.