Nchi za Kiarabu zatoa wito wa kusitisha vita Gaza na Lebanon
11 Novemba 2024Viongozi wa Umoja wa nchi za Kiarabu na wale waliopo kwenye Jumuiya ya Kiislamu wamekusanyika hivi leo katika mji mkuu wa Saudia - Riyadh, kujadili mzozo unaoendelea kupamba moto katika eneo la Mashariki ya Kati ikiwa ni zaidi ya mwaka mmoja Israel ikipambana na wanamgambo wa Hamas huko Gaza na pia wale wa Hezbollah nchini Lebanon.
Akiufungua mkutano huo, mtawala wa Saudi Arabia mwanamfalme Mohammed bin Salman amesema jumuiya ya kimataifa inapaswa kukomesha mara moja vitendo vya Israel huko Palestina na Lebanon.
Soma pia: Viongozi wa Kiarabu na Kiislamu wakutana Saudia kujadili mzozo wa Mashariki ya Kati
"Ufalme wa Saudia unapinga vikali mauaji ya halaiki yanayofanywa na Israel dhidi ya watu wa Palestina ambao ni ndugu zetu, mauaji ambayo yamesababisha vifo vya zaidi ya mashahidi 150,000 na wengine wakijeruhiwa, wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto," alisema Bin Salman.
Ikumbukwe tu kwamba vita kati ya Israel na Hamas vilivyoanza Oktoba 7 mwaka jana, tayari vimesababisha vifo vya watu zaidi ya 43,600 hadi sasa.
Mvutano kati ya Israel na Iran wajadiliwa
Mwanamfalme Bin Salman ameendelea kuwa Saudi Arabia inathibitisha uungaji wake mkono kwa Palestina na Lebanon ili kukabiliana na matokeo mabaya ya kibinadamu yanayosababishwa na uvamizi unaoendelea wa Israel. Pia, mwanamfalme huyo amesisitiza kuwa Israel inapaswa kuheshimu uhuru wa Iran na kuachana kabisa mipango yoyote ya kuishambulia Tehran.
Rasimu ya azimio la mkutano huo inasisitiza pia uungaji mkono madhubuti kwa "haki za kitaifa na uhuru" kwa watu wa Palestina, bila kusahau suluhisho la mataifa mawili.
Hata hivyo, saa chache kabla ya hapo, Waziri mpya wa Mambo ya Nje wa Israel Gideon Saar amesema kwa sasa ni mapema mno kufikiria wazo la kuanzisha taifa la Palestina ambalo amelitaja kwamba litakuwa ni taifa la Hamas.
Kauli ya serikali ya Lebanon katika mkutano huo
Waziri Mkuu wa Lebanon Najib Mikati amehutubia pia mkutano huo wa nchi za Kiarabu na Kiislamu uliofanyika mjini Riyadh na kwanza ameyataka mataifa kadhaa kutoingilia masuala yake ya ndani huku akiitolewa wito jumuiya ya kimataifa kuiunga mkono serikali yake na si makundi yanayoendesha harakati zao nchini humo.
" Kwa hivyo, ninakuombeni kwa dhati kuiunga mkono serikali ya Lebanon na taasisi zake huru za kikatiba na za kifedha, na pia kuendelea kutuma misaada ya haraka ya kibinadamu, chakula na vifaa vya matibabu, " amesisitiza Mikati.
Mapema leo, Israel imesema kumekuwa na "maendeleo chanya" katika juhudi za kumaliza mapigano nchini Lebanon, lakini msemaji wa kundi wanamgambo wa Hezbollah amekanusha taarifa hiyo na kusema hawajapokea pendekezo lolote rasmi na kwamba wako tayari kuendesha vita vya muda mrefu ikiwa itahitajika.
(Vyanzo: AP, DPAE, RTRE, AFP)